Serikali ya Somalia yapiga marufuku maandamano ya wapinzani
Serikali ya Somalia imetangaza kupiga marufuku maandamano ya wapinzani katika mji mkuu Mogadishu kutokana na ongezeko la maambukizi ya ya corona na tishio la usalama.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Hassadn Hundubey Jima'le amesema maandamano Mogadishu yawe ni ya kupinga serikali au ya kuunga mkono serikali ni kinyume cha sheria.
Tangazo hilo limekuja baada ya wapinzani wanaogombea urais wakiongozwa na rais wa zamani Shariff Sheikh Ahmed kusema wataendelea kuandamana huku wakisema maandamano mapya yatafanyika Ijumaa.
Kiongozi wa upinzani Ali Hassan, ameituhumu serikali, kwa kutumia mali ya umma kuwahangaisha waandamanaji wanaopinga kusalia kwake madarakani, badala ya kununua hewa ya oxygen inayohitajiwa na wagonjwa wa Corona.
Muhula wa rais wa sasa Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmaajo, ulimalizika Februari 8 lakini kutokana na mgogoro wa kisiasa, bunge linalomchagua rais bado halijachaguliwa.
Wakati huo huo serikali ya Somalia imetangaza kufunga shule zote na vyuo vikuu kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona nchini humo, hatua ambayo imeafikiwa baada ya mkutano wa bazara la mawaziri.
Hadi sasa Somalia imesajili visa 6,246 vya maambukizi ya Corona, pamoja na vifo 208.