Katibu Mkuu wa UN ana wasiwasi kuhusu mkwamo wa kisiasa Somalia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mkwamo wa kisiasa unaondelea nchini Somalia kuhusu uchaguzi mkuu licha ya kufanyika duru kadhaa za majadiliano miongoni mwa wadau wa kisiasa nchini humo katika ngazi zote ni suala linalomtia wasiwasi mkubwa.
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani Katibu Mkuu amesema kuendelea kwa mkwamo huo wa kisiasa kwa muda mrefu kuna hatarisha utulivu wa taifa hilo la Pembe ya Afrika na mustakbali wa watu wa Somalia ambao tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu na mazingira tete ya usalama.
Guterres ameitaka serikali ya Kifederali ya Somalia na viongozi wa majimbo kujihusisha katika mazungumzo na kupanga mkutano wa dharura bila masharti ili kutatua tofauti zao kuhusu mchakato wa uchaguzi na kufikia muafa wa jinsi ya kusonga mbele.
Pia amekaribisha ahadi ya viongozi wa Somalia ya tarehe 17 Septemba kuhusu muundo wa uchaguzi na kuwatolea wito wa kuafiki haraka utekelezaji wake na kufanya uchaguzi bila kuchelewa.
Katibu Mkuu amerejea kusema kwamba Umoja wa Mataifa umejizatiti kuisaidia Somalia kuelekea amani, utulivu na mafanikio.
Taifa hilo la Pembe ya Afrika lilipaswa kufanya uchaguzi wake wa rais Februari 8, lakini hilo halikufanyika kufuatia mvutano kati ya serikali kuu na majimbo kukosa kukubaliana kuhusu jinsi ya kuendelea mbele na uchaguzi.
Kulingana na makubaliano ya awali, uchaguzi wa bunge Somalia ungefanyika mwezi Desemba mwaka 2020 na wa rais ungefanyika mapema mwaka 2021.
Hatua ya kutofanya uchaguzi imeiweka Somalia katika hali tete kisiasa, wakati nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko la mashambulizi ya magaidi, uvamizi wa nzige, uhaba wa chakula na janga la corona.