Kongo Brazzaville kuimarisha uhusiano na marafiki zake
Jamhuri ya Kongo Brazzaville imesema kuwa, itaendelea kuwa na uhusiano mzuri na marafiki zake, na kwamba mashinikizo ya kigeni hayataifanya nchi hiyo iwasahau marafiki zake.
Hayo yamesemwa na Jean Claude Gakosso, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo wakati alipoonana na wanadiplomasia wa kigeni mjini Brazzaville na kusisitiza kuwa, nchi yake ina hamu ya kuona uhusiano wake na marafiki zake unaimarika katika misingi ya kuheshimiana, kufanya kazi kwa pamoja, urafiki na kuwa kitu kimoja.
Hivi karibuni pia, Rais Denis Sassou N'Guesso wa Kongo Brazzaville alisisitiza kuwa, siasa za nchi yake ni kutangulia kuchukua hatua za kuimarisha uhusiano na marafiki zake kwani anaamini kuwa maendeleo ya nchi hiyo hayawezi kupatikana bila ya kushirikiana kwa karibu na nchi marafiki.
Hata hivyo matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Kongo Brazzaville yanaonekana yameukasirisha Umoja wa Ulaya na Marekani kwani balozi wa Umoja wa Ulaya, Saskia De Lang pamoja na balozi wa Marekani, Stéphanie Sullivan waliondoka kwenye kikao hicho kabla ya kumalizika hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo.