Viongozi wa Uamsho Zanzibar wafutiwa kesi, waanza kuondoka gerezani
(last modified Wed, 16 Jun 2021 12:26:42 GMT )
Jun 16, 2021 12:26 UTC
  • Viongozi wa Uamsho Zanzibar wafutiwa kesi, waanza kuondoka gerezani

Viongozi 36 wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), wakio gozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi, wameachiwa huru.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Tanzania, Sylvester Mwakitalu amewafutia mashtaka viongozi wote wa jumuiya hiyo na kwamba kilichobaki sasa ni taratibu za kutoka gerezani.

Wawili hao ambao  walikuwa mahabusu tangu mwaka 2014 pamoja na wenzao kutokana na kukabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana wameachiwa huru jana Jumanne Juni 15, 2021  baada ya DPP kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Katika ufafanuzi wake  Mwakitalu amesema, “ni kweli wameachiwa huru. Nimewafutia wote mashtaka yaliyokuwa yanawakabili. Sasa suala la kutoka gerezani kama wameshatoka wote au wangapi hilo ni suala la taratibu za Magereza lakini mimi nimewafutia mashtaka  wote.”

Washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya 2002 Januari 2013 na Juni 2014.

Waislamu visiwani Zanzibar wakifuatilia hotuba za Ijumaa

Awali walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam  kwa hatua za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji kamili wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 25.

Lakini Aprili 23, 2021 Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka 14 baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wao, Daimu Halfani, Juma Nassoro, Jeremiah Mtobesya na  Abubakar Salum kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo kwa kuwa makosa wanayotuhumiwa yanadaiwa kutendeka Zanzibar.