EU kuiondolea Burundi vikwazo, mchakato umeanza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71560-eu_kuiondolea_burundi_vikwazo_mchakato_umeanza
Umoja wa Ulaya umeanzisha mchakato wa kuiondolea Burundi vikwazo ambavyo vilifunga kabisa mlango wa kupewa misaada serikali ya Bujumbura.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Jun 23, 2021 02:26 UTC
  • EU kuiondolea Burundi vikwazo, mchakato umeanza

Umoja wa Ulaya umeanzisha mchakato wa kuiondolea Burundi vikwazo ambavyo vilifunga kabisa mlango wa kupewa misaada serikali ya Bujumbura.

Hayo yamesemwa na Claude Bochu, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Burundi ambaye ameongeza kuwa, EU pamoja na washirika wake wengine kama Benki ya Ustawi ya Afrika (ADB) watafadhili mpango wa kufufua Bandari ya Bujumbura kufikia mwishoni mwa mwaka huu. 

Ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya umepanga kufadhili sekta ya kilimo ya Burundi, hatua ambayo inatazamiwa kupiga jeki usalama wa chakula nchini humo.

Machi mwaka 2016, EU ilisimamisha misaada yake yote kwa serikali ya Burundi, kutokana na kile ilichodai kuwa ni mgogoro wa kisiasa uliozuka baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kutangaza kuwa atagombea muhula wa tatu wa urais.

Hayati Nkurunziza aliyeaga dunia mwaka jana kwa 'mshtuko wa moyo'

Serikali ya Burundi chini ya uongozi wa hayati Nkurunziza iliandamwa na tuhuma nyingi za kufanya ukandamizaji mkubwa wa umwagaji wa damu dhidi ya wapinzani katika kona mbalimbali za Burundi.

Hata hivyo hali ya haki za binadamu na usalama katika nchi hiyo imeanza kuboreka chini ya utawala wa rais wa sasa wa nchi hiyo Evariste Ndayishimiye.