DRC: Madai kuwa tumepokea silaha kutoka Korea Kaskazini ni kichekesho
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7171-drc_madai_kuwa_tumepokea_silaha_kutoka_korea_kaskazini_ni_kichekesho
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepuuzilia mbali ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyodai kuwa nchi hiyo imekuwa ikipokea silaha kutoka Korea Kaskazini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 16, 2016 07:50 UTC
  • DRC: Madai kuwa tumepokea silaha kutoka Korea Kaskazini ni kichekesho

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepuuzilia mbali ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyodai kuwa nchi hiyo imekuwa ikipokea silaha kutoka Korea Kaskazini.

Msemaji wa serikali Lambert Mende ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, madai hayo ni ya uwongo na wala hayana msingi wowote. Amesema nchi hiyo haijawahi kufanya ushirikiano wowote na Korea Kaskazini tangu baada ya kuaga dunia rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Kabila, mwaka 2001.

Umoja wa Mataifa ulikosoa kile kilichotajwa kuwa hatua ya Korea Kaskazini kutuma silaha kwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ripoti iliyotolewa na wataalamu wa tume inayofuatilia vikwazo vya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa, silaha zinazotumwa kwa jeshi la serikali ya Kinshasa na zile zinazotumwa kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, zinafanana sana na silaha zinazoundwa Korea Kaskazini. Aidha ripoti hiyo iliongeza kuwa, silaha hizo ziliingizwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 2014, wakati wa kupewa mafunzo gadi ya rais na polisi ya nchi hiyo na kwamba ziliingizwa na makamanda 30 wa Korea Kaskazini waliokuwa wametumwa kusimamia mafunzo hayo. Kwa mujibu wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, serikali ya Pyongyang na jeshi lake hairuhusiwi kuuza, kununua au kutoa mafunzo ya kijeshi kwa nchi nyingine.