Maandamano ya wiki hii ya wananchi wa Algeria yalikuwa ni ya Ijumaa ya 124
(last modified Sun, 04 Jul 2021 02:37:25 GMT )
Jul 04, 2021 02:37 UTC
  • Maandamano ya wiki hii ya wananchi wa Algeria yalikuwa ni ya Ijumaa ya 124

Wananchi wa Algeria wanaendelea na maandamano yao ya kila wiki ambapo maandamano yaliyofanyika Ijumaa wiki hii, yalikuwa ya 124 ya kutaka mabadiliko ya kimsingi ya mfumo wa kisiasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, waandamanaji nchini Algeria wameshiriki kwa wingi katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo ikiwa ni kuendeleza harakati ya wananchi ya kufanikisha malengo yao ya kutimuliwa madarakani mabaki yote ya viongozi wa serikali ya Abdulaziz Bouteflika aliyelazimika kuondoka madarakani kutokana na mashinikizo makubwa ya wananchi.

Katika maandamano ya wiki hii, wananchi wa Algeria walibeba picha za wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo na kupiga mayowe ya kutaka waachiliwe huru wafungwa hao.

Harakati ya wananchi wa Algeria iliundwa mwaka 2019 kwa ajili ya kupinga jaribio la Bouteflika la kugombea tena urais wa nchi hiyo licha ya kwamba alikuwa mgonjwa asiyeweza kutembea mwenyewe bila ya msaada wa kigari cha wagonjwa. Bouteflika alitaka kugombea tena urais wa Algeria kwa kipindi cha tano mfululizo.

Licha ya kushindwa hata kutembea, lakini Bouteflika alitaka kugombea tena urais kwa mara ya tano

 

Maandamano ya amani ya wananchi wa Algeria yalipelekea kung'oka madarakani Bouteflika katikati ya mwaka 2019. Hata hivyo maandamano hayo ya wananchi wa Algeria yalitekwa na mabaki ya watawala wa serikali yake na sasa hivi wananchi wa nchi hiyo wanawalaumu viongozi wa hivi sasa kwa kupanda mawimbi ya maandamano yao na kutwaa madaraka kinyume na malengo ya wananchi wa Algeria.

Ni kwa sababu hiyo ndio maana kila Ijumaa, wananchi wa Algeria wanaendelea kumiminika mabarabarani kushinikiza kufutwa mabaki yote ya viongozi wa serikali ya Bouteflika. Kama tulivyosea, maandamano ya Ijumaa ya wiki hii yalikuwa ni ya 124.