Magaidi 50 wa kundi la al-Shabab Somalia waangamizwa na jeshi
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, magaidi wasiopungua 50 wa kundi la al-Shabab wameangamizwa kufuatia shambulio la anga dhidi ya ngome zao katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Taarifa ya jeshi la Somalia imeeleza kuwa, magaidi hao wa kundi la wanamgambo wa al-Shabab wameangamizwa katika mkoa wa Galmudug ambapo watatu kati ya waliouawa ni magaidi kutoka nje. Hata hivyo taarifa ya jeshi la Somalia halijataja uraia wa magaidi hao.
Shambulio hilo la anga la jeshi la Somalia limefanyika sambamba na operesheni ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo dhidi ya ngome za wanamgambo wa al-Shabab inayoendelea katika mji huo wa Galmudug.
kadhalika jeshi la Somalia limetangaza pia kuwa, ngome za al-Shabab katika maeneo hayo zimeharibiwa kabisa huku wanamgambo wengine wa kundi hilo wakilazimika kukimbia baada ya kuzidiwa nguvu na na wanajeshi wa Somalia.
Itakumbukwa kuwa, majuzi tu jeshi la Somalia lilitangaza kuwa, limewauwa wanamgambo 15 wa kundi la kigaidi la al-Shabab katika operesheni yake ya kijeshi liliyoifanya katika vijiji na miji ya kusini mwa nchi hiyo.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qeida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.