Aug 01, 2021 07:51 UTC
  • Wanachama 91 wa Boko Haram wajisalimisha kwa jeshi la Nigeria

Wanachama 91 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamejisalimisha kwa jeshi la Nigeria huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Naibu Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria, Bernard Onyeuko amesema kuwa magaidi 91 wa genge hilo walijisalimisha kufuatia operesheni iliyofanywa na vitengo vya jeshi katika maeneo tofauti katika jimbo la Borno.

Onyeuko amesema kuwa idadi kubwa ya silaha na zana za kivita za wanachama wa kundi hilo la ukufurishaji zimekamatwa pia katika operesheni hiyo.

Ameongeza kuwa, kwa sasa washukiwa hao wanafanyiwa uchunguzi ili kujua namna kesi zao zitakavyoendeshwa kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa.

Abubakar Shekau, kinara wa Boko Haram aliyeuawa (kujiua) hivi karibuni

Mapema mwezi uliopita wa Julai, Jenerali Onyeuko alisema magaidi wasiopungua 73 wa Boko Haram wameuawa katika operesheni ya maafisa usalama dhidi ya kundi hilo katika miji tofauti ya jimbo la Borno baina ya Juni 18-30.

Zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika hujuma za Boko Haram tokea mwaka 2009 katika nchi nne za magharibi mwa Afrika za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon, na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi hayo.

 

Tags