Raia 125 wauawa katika hujuma ya waasi kaskazini mwa Ethiopia
(last modified Thu, 09 Sep 2021 09:49:30 GMT )
Sep 09, 2021 09:49 UTC
  • Raia 125 wauawa katika hujuma ya waasi kaskazini mwa Ethiopia

Madaktari wa Ethiopia wamethibitisha kuwa raia wasiopungua 125 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa kundi la TPLF huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na madaktari hao imesema kuwa waasi wa kundi la Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wameua raia wasiopungua 125 katika eneo la Amhara lililoko kaskazini mwa Ethiopia.

Kundi la TPLF ambalo sasa linatambuliwa kuwa kundi la kigaidi nchini Ethiopia liimekuwa likitekeleza mashambulio yasiyokoma katika majimbo na mikoa ya kaskazini ya Amhara na Afar.

Hadi sasa mapigano kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na waasi wa harakati ya TPLF yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula. 

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.