13 watiwa mbaroni Rwanda wakituhumiwa kupanga mashambulio ya "kigaidi"
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75298-13_watiwa_mbaroni_rwanda_wakituhumiwa_kupanga_mashambulio_ya_kigaidi
Polisi ya Rwanda imesema, imewatia mbaroni watu 13 wanaoshukiwa kupanga mashambulio ya "kigaidi" dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Kigali na kuwaonyesha watuhumiwa hao kwa vyombo vya habari.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 02, 2021 07:41 UTC
  • 13 watiwa mbaroni Rwanda wakituhumiwa kupanga mashambulio ya

Polisi ya Rwanda imesema, imewatia mbaroni watu 13 wanaoshukiwa kupanga mashambulio ya "kigaidi" dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Kigali na kuwaonyesha watuhumiwa hao kwa vyombo vya habari.

Taarifa iliyotolewa na Polisi ya Taifa ya Rwanda imesema, watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na vifaa kadhaa vya kutengeneza mabomu zikiwemo mada za miripuko, nyaya, misumari na simu za mkononi.

"Uchunguzi umeonyesha kuwa kikundi hicho cha kigaidi kilikuwa kikifanya kazi kwa kushirikiana na Vikosi vya Muungano wa Kidemokrasia (ADF)", imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Polisi ya Rwanda ikimaanisha kundi hilo la kigaidi linaloendesha harakati zake mashariki mwa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi wa ADF

ADF, ambalo kihistoria ni kundi la waasi wa Uganda, limekuwa likituhumiwa kuhusika na mauaji ya maelfu ya raia katika eneo la mashariki ya Kongo DR.

Msemaji wa Polisi ya Rwanda amesema, mtuhumiwa wa kwanza wa kikundi cha watu hao 13 alitiwa nguvuni mwezi Agosti na watuhumiwa wengine walikamatwa mwezi uliopita wa Septemba.../