Oct 04, 2021 04:12 UTC
  • 24 wauawa katika mapigano baina ya Boko Haram na ISWAP Nigeria

Kundi la kigaidi la Boko Haram limeua wapiganaji 24 wa kundi hasimu la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu la Mkoa wa Afrika Magharibi (The Islamic State West Africa Province) kwa kifupi ISWAP, huko kaskazini mwa Nigeria.

Duru za habari zinaarifu kuwa, wanachama hao wa ISWAP waliuawa jana Jumamosi katika makabiliano na Boko Haram katika milima ya Mandra na Gaba, eneo la Gwoza lililoko katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi.

Inaarifiwa kuwa, wanachama wa Boko Haram chini ya uongozi wa Aliyu Ngulde, waliwashambulia wafuasi wa ISWAP walioukuwa wakiongozwa na Abou Aseeya katika eneo hilo na kuwaua.

Habari zaidi zinasema kuwa, katika makabiliano baina ya makundi hayo hasimu ya kigaidi, wanachama kadhaa wa ISWAP walishikwa mateka na wapiganaji wa Boko Haram.

Wanachama wa genge la kigaidi la ISWAP

Magaidi wa Boko Haram mbali na kutekeleza wimbi la hujuma dhidi ya genge la ISWAP tokea mwezi Juni mwaka huu baada ya kuuawa kiongozi wao Abu Bakar Shekau, lakini wameshadidisha pia mashambulio yao dhidi ya wanajeshi na raia wa nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni. 

Mamia ya wanajeshi wa Nigeria wameuawa na wanachama wa Boko Haram tangu mwezi Januari mwaka huu 2021.

ISWAP ni tawi lililojitenga na kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo lilianzisha uasi nchini Nigeria mwaka 2009 na hatimaye kupanua hujuma na mashambulio yake ya kigaidi katika nchi jirani zinazopakana na Ziwa Chad, za Cameroon, Niger na Chad.

Tags