UN: Wakimbizi wa Burundi na DRC walioko Rwanda wanahitaji msaada
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7591-un_wakimbizi_wa_burundi_na_drc_walioko_rwanda_wanahitaji_msaada
Umoja wa Mataifa umesema wakimbizi raia wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioko nchini Rwanda wanahitajia misaada ya dharura na kwamba idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini humo kutoka nchi mbili hizo na haswa Burundi ni ya kutia wasi wasi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2016 11:52 UTC
  • UN: Wakimbizi wa Burundi na DRC walioko Rwanda wanahitaji msaada

Umoja wa Mataifa umesema wakimbizi raia wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioko nchini Rwanda wanahitajia misaada ya dharura na kwamba idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini humo kutoka nchi mbili hizo na haswa Burundi ni ya kutia wasi wasi.

Erika Fitzpatrick, Ofisa wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR nchini Rwanda amesema kuwa, idadi ya wakimbizi kutoka nchi mbili hizo inapindukia 152,200 na kwamba serikali ya Kigali inahitaji zaidi ya dola milioni 94.5 za Marekani ili kukidhi mahitaji ya kila siku ya wakimbizi 77,678 wa Burundi na dola milioni 35.9 kwa ajili ya kuyashughulikia mahitaji ya wakimbizi 74,587 wa Kongo DR.

Ameongeza kuwa, kufikia sasa wameweza kukusanya dola milioni 16 pekee huku akitoa wito kwa wafadhili kujitokeza na kutoa misaada yao kabla ya Siku ya Wakimbizi Duniani mwezi ujao wa Juni. Amesema kwa wastani Warundi 25 wanaingia nchini Rwanda kila siku kutafuta hifadhi.

Haya yanajiri katika hali ambayo, mazungumzo ya kuukwamua mzozo wa kisiasa nchini Burundi huko mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, yameanza bila kuhudhuriwa na muungano mkuu wa upinzani, jambo ambalo linazidi kuzima matumaini ya kupatikana amani nchini humo.

Machafuko nchini Burundi yaliibuka mwezi Aprili mwaka jana, baada ya chama tawala CNDD-FDD kuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea kwa mara ya tatu mfululizo kwenye uchaguzi mkuu uliopita, machafuko ambayo mbali na vifo, yamesababisha maelfu ya wananchi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.