Maandamano ya wananchi dhidi ya mapinduzi ya kijeshi yanaendelea nchini Sudan
(last modified Sun, 31 Oct 2021 02:21:55 GMT )
Oct 31, 2021 02:21 UTC
  • Maandamano ya wananchi dhidi ya mapinduzi ya kijeshi yanaendelea nchini Sudan

Mamilioni ya wananchi wa Sudan wameendelea kufanya maandamano katika miji ya Sudan na miji mingine 50 ya kona mbalimbali za dunia ili kutangaza upinzani wao dhidi ya mapinduzi ya kijeshi nchhini humo.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza kuwa, maandamano ya wananchi yameendelea katika miji mbalimbali ya Sudan ukiwemo mji mkuu Khartoum. Kwa mujibu wa televisheni hiyo, mbali na Khartoum, maandamano hayo yamefanyika pia katika miji mingine 25 ndani ya Sudan na 50 ya nchi mbalimbali duniani. Maandamano hayo yote ni ya kushinikiza kung'oka madarakani Abdul Fattah al Burhan, kamanda wa jeshi aliyefanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya mpito ya Sudan ambayo ilishirikisha pia raia.

Waandamanaji hao wametangaza hadharani kuwa wanataka majenerali wa kijeshi warejee kwenye kambi zao, serikali ya kiraia irudi madarakani, wanasiasa waliokamatwa waachiliwe huru na Katiba itawale katika masuala yote ya Sudan.

Aidha wananchi hao wenye hasira nchini Sudan wameapa kuendeleza maandamano na kuendesha kampeni ya uasi wa kiraia, baada ya waandamanaji kadhaa kuuawa katika maandamano hayo.

Jenerali Abdul Fattah al Burhan aliyefanya mapinduzi ya kijeshi nchni Sudan

 

Watu wasiopungua wanane wameshauawa na wengine 170 wamejeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika nchini Sudan tangu jeshi liliponyakua madaraka kwa nguvu Jumatatu iliyopita. Kwa mujibu wa duru za tiba, mwandamanaji mwengine mmoja ameuawa wakati askari usalama walipofyatua gesi ya kutoa machozi na risasi hai na za plastiki dhidi ya waandamanaji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelihimiza jeshi la Sudan kuwa na stahamala na kutosababisha maafa zaidi kwa raia, akisema kuwa, jeshi la Sudan linapaswa kuruhu watu kuandamana kwa amani kwani hiyoi ni haki yao.

Tags