Waethiopia wailaani Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao
Wananchi wa Ethiopia wamefanya maandamano makubwa ya kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed na jeshi la nchi hilo linalokabiliana na waasi wa eneo la Tigray; huku wakiikosoa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.
Katika maandamano hayo yaliyofanyika jana Jumapili, wananchi wa Ethiopia wamekosoa mwito uliotolewa na Washington wa kuitaka serikali ya Addis Ababa ifanye mazungumzo na waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).
Mmoja wa waandamanaji hao, Tigist Lemma (37) amenukuliwa akisema, "Mbona Marekani hawafanyi mazungumzo na magaidi kama al-Shabaab? Wanataka kusambaratisha nchi yetu kama walivyofanya huko Afghanistan, lakini kamwe hawatafanikiwa, hii ni Ethiopia."
Akthari ya waandamanaji hao waliokuwa wamekusanyika katika Medani ya Meskel jijini Addis Ababa, walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kuukashifu utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani. Baadhi ya jumbe hizo zilisema "Aibu kwako Marekani" na "US acha kufyonza damu ya Waethiopia."
Waasi nchini Ethiopia wakiwemo wale wa kundi la Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wameafiki kuunda muungano dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed huku duru zikiarifu kuwa wako nje ya mji mkuu Addis Ababa wakilenga kuuteka.
Mzozo wa mwaka mzima sasa kati ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho ya Ethiopia na waasi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi umepelekea kuuawa maelfu ya watu na kulazimisha wengine zaidi ya milioni 2.5 kuwa wakimbizi.