Wananchi wa Sudan waandamana usiku wakipinga utawala wa kijeshi
Wananchi wa Sudan wamefanya maandamano usiku wa kumkia leo wakilalamikia mapinduzi ya kijeshi ya nchi hiyo na hatua ya Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan ya kuunda Baraza la Utawala.
Maandamano hayo yaliyofanyika katika miji mbalimbali ya Sudan yametoa wito wa kuhitimishwa utawala wa kijeshi na badala yake kuundwa utawala wa kiraia.
Wakiwa wamebeba mabango na maberamu yenye jumbe na maandishi mbalimbali kama "Hapana, kwa mapinduzi ya kijeshi" na "demokrasiia itarejea" walisikika wakipiga nara dhidi ya Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi mkuu wa mapinduzi ya Oktoba 25, alitangaza Baraza jipya la Utawala Alkhamisi ya juzi Novemba 11. Viongozi kadhaa ambao walidai madaraka kukabidhiwa kwa raia hawakushirikishwa katika baraza hilo.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anaendelea kuwa mwenyekiti wa Baraza hili jipya la Utawala. Kiongozi nambari mbili pia anaendelea kuwa Jenerali Mohammed Hamdan Dogolo, anayejulikana kama "Hemedti", kiongozi mwenye nguvu ambaye Vikosi vya Msaada wa Haraka vilishutumiwa kwa unyanyasaji wakati wa maandamano yaliyosababisha kuanguka kwa utawala wa Omar al-Bashir.
Kati ya watu kumi na wanne katika baraza hili, ni majina kumi na tatu pekee ambayo yametangazwa. Kiongozi anayetakiwa kuwakilisha mashariki mwa nchi hajateuliwa kwenye baraza hilo.
Mabadiliko makubwa ni kuondolewa kwa wawakilishi wanne wa muungano wa Forces for Freedom and Change (FFC), ambao ulikuwa ukidai madaraka yakabidhiwe raia.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umewataka watawala nchini Sudan kuheshimu maandamano ya amani ya raia wa nchi hiyo na kujiepusha na vitendo vya ukandamizaji dhidi yao.