UN: Mauaji ya waandamanaji Sudan ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mauaji ya watu 39 nchini Sudan yaliyofanywa na vikosi vya ulinzi tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi nchini humo tarehe 25 Oktoba mwaka huu.
Watu 15 kati yao wameripotiwa kupigwa risasi siku ya Jumatano pekee wakati wa maandamano yaliyofanyika mjini Khartoum, Khartoum-Bahri na Omdurman.
Michelle Bachelet ameeleza katika taarifa, "kufuatia wito wetu wa mara kwa mara kwa jeshi na mamlaka za usalama kuacha kutumia nguvu zisizo za lazima na zisizo na uwiano dhidi ya waandamanaji, ni aibu sana na jambo la kusikitisha kwamba risasi za moto zimetumika tena dhidi ya waandamanaji. Ufyatuaji risasi kwenye umati mkubwa wa waandamanaji wasio na silaha, na kuacha watu kadhaa wakiwa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa, ni jambo la kusikitisha, ambalo linalenga kuzima sauti ya upinzani wa umma, na huo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu."
Kwa mujibu wa duru za utoaji huduma za tiba, zaidi ya watu 100 walijeruhiwa wakati wa maandamano ya Jumatano na 80 kati yao walipata majeraha ya risasi kwenye miili yao sehemu ya juu na vichwani.
Katika taarifa yake hiyo, Bi Bachelet ameeleza pia kwamba, kuzimwa kwa mawasiliano kunamaanisha kuwa watu hawawezi kupiga simu kwa huduma za magari ya kubeba wagonjwa ili kuwatibu waandamanaji waliojeruhiwa, familia haziwezi kuangalia usalama wa wapendwa wao, na hospitali haziwezi kufikia madaktari kwani vyumba vya dharura vimejaa; na akaongezea kwa kusema, kuzimwa kwa mtandao na mawasiliano kwa ujumla ni kukiuka kanuni za msingi za umuhimu wa haja ya mawasiliano na ni kukiuka sheria za kimataifa.
Ripoti kutoka Sudan zinaonyesha kuwa, waandishi wa habari pia wamekuwa wakikamatwa, kushambuliwa wakati wakiripoti na pia nyumba na ofisi zao kupekuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama.
Katika taarifa yake, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza pia kuwa, maafisa wa vikosi vya usalama pamoja na viongozi wa kisiasa na kijeshi wanaohusika na matumizi ya nguvu kupita kiasi na yasiyo na uwiano dhidi ya waandamanaji lazima wawajibishwe kwa kuzingatia sheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.../