Wasudan washinikiza wanajeshi warudi makambini, kuundwe serikali ya raia
(last modified Fri, 26 Nov 2021 02:48:46 GMT )
Nov 26, 2021 02:48 UTC
  • Wasudan washinikiza wanajeshi warudi makambini, kuundwe serikali ya raia

Wananchi wa Sudan wameendelea na maandamano yao wakishinikiza wanajeshi warudi makambini ili waruhusu kuundwa serikali ya kiraia na ya kidemokrasia nchini humo.

Televisheni ya Rusia al Yaum imeripoti kuwa, maandamano ya wananchi wa Sudan yaliendelea tena jana Alkhamisi katika mji mkuu Khartoum na miji mengine ili kupinga mapambano yaliyofikiwa baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongozwa na Abdul Fattah al Burhan, na Abdulla Hamdok, waziri mkuu wa Sudan aliyepinduliwa na baadaye kurejeshwa tena madarakani.

Taarifa zinasema kuwa, maelfu ya wananchi wa Sudan wameshiriki kwenye maandamano hayo wakiendelea kutoa mwisho wa kuundwa serikali ya kiraia, kupinga mapinduzi ya kijeshi na kutaka wanajeshi warudi makambini mwao.

Maandamano hayo yamekuja siku chache tu baada ya jeshi kutia saini makubaliano ya kuwashirikisha raia katika uongozi baina yake na Waziri Mkuu Abdallah Hamdok kulikopelekea waziri mkuu huyo arejee madarakani baada ya kupinduliwa na wanajeshi karibu mwezi mmoja uliopita.

Maandamano ya wananchi yanaendelea Sudan kushinikiza wanajeshi warejee makambini ili waruhusu kuundwa serikali ya kidemokrasia

 

Waandamanaji ambao walikuwa wamebeba bendera za Sudan wamepiga nara za "Wananchi wanataka kupinduliwa utawala wa kijeshi" na "Laana kwa wanajeshi."

Sudan imekumbwa na mgogoro tangu wakati wa maandamano yaliyomg'oa madarakani Jenerali Omar al Bashir ambapo majenerali wa kijeshi nchini Sudan walitumia vibaya fursa ya maandamano ya wananchi, kufanya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2019 na kumg'oa madarakani Omar al Bashir na baaadaye kung'ang'ania wao madaraka.

Juzi Jumatano Abdalla Hamdok aliwaambia waandishi wa habari kuwa kama watu wote waliowekwa kizuizini na wanajeshi hawatoachiliwa huru, basi makubaliano yake na wanajeshi hayatokuwa na maana yoyote.

Tags