Shambulio jipya la waasi laua watu 33 Jamhuri ya Afrika ya Kati
Watu wapatao 33, wakiwemo wanajeshi wawili, wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa kwa wakati mmoja na watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa waasi wa kundi liitwalo 3R katika vijiji viwili vilivyoko kaskazini magharibi mwa mkoa wa Ouham-Pendé, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa hiyo ni idadi kubwa zaidi ya watu waliopoteza maisha tangu Rais Faustin Archange Touadéra atangaze kusitishwa mapigano nchini humo katikati ya mwezi Oktoba.
Shambulio hilo ambalo limeripotiwa kuwa lilitokea Jumatatu wiki hii, limehusishwa na waasi wa kundi la 3R ambao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji mengi yanayoendelea kutokea katika eneo hilo.
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA vinalishutumu pia kundi hilo la wabeba silaha kwa kuwaua raia 12 siku chache zilizopita.
Kulingana na ushahidi uliokusanywa na maafisa wa serikali ya Bangui, waasi hao walianzisha mashambulizi ya kushtukiza kuanzia saa kumi alfajiri siku ya Jumatatu ambapo kundi moja liliwashambulia wanajeshi wa serikali wa FACA huku kundi lingine likiwashambulia raia katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Ouham-Pendé washambuliaji hao hatimaye walirudi msituni mwendo wa saa nne asubuhi, na kuacha miili ya raia 29 waliouawa kinyama huko Kaïta, ikiwa ni pamoja na raia wengine 2 na wanajeshi wawili waliouawa eneo la Boy-ngou.
Itakumbukwa kuwa mnamo katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadera alitangaza uamuzi wa kusitisha vita na makundi ya waasi huku akielezea matumaini yake kuwa hatua hiyo itapelekea kuanza mazungumzo ya amani nchini humo.../