Saiful Islam Gaddafi kukatiza ndoto ya Khalifa Haftar ya kutawala Libya?
Kurejea kwa Saif al-Islam Gaddafi katika kinyang'anyiro cha urais, kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Sabha (kusini mwa Libya), kumechanganya tena karata nchini Libya, hasa kutokana na kukithiri kwa mizozo na mivutano kati yake na Jenerali mstaafu, Khalifa Haftar katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Ni baada ya mahakama moja ya kusini mwa Libya kutoa idhini Saif al Islam, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi, agombee urais katika uchaguzi wa tarehe 24 mwezi huu wa Disemba. Mahakama ya Sebha imesikiliza kesi iliyofunguliwa na Saif al Islam Gaddafi ya kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Libya wa kumkatalia kugombea urais nchini humo mwezi uliopita.
Uadui baina ya wafuasi wa utawala wa zamani wa Libya na waungaji mkono wa Haftar, uliibuka tena baada ya jenerali huyo mstaafu kufunga Mahakama ya Sabha kwa siku kadhaa kwa nguvu ya silaha, ili kumzuia wakili wa Saif al-Islam kuwasilisha rufaa yake dhidi ya kuenguliwa mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya kwenye uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Desemba 24.

Wafuasi wa Saif al-Islam Gaddafi walijitokeza katika mji wa Sabha na katika miji mingine ya Libya, wakishangilia kwa kurejea kwake kwenye kinyang'anyiro cha urais, jambo ambalo linaweza kukatisha matumaini ya Haftar kushika madarakani kwa sababu ya utegemezi wake kwa wafuasi wa utawala wa zamani katika vikosi vyake na kwa ajili ya kupata kura katika uchaguzi ujao.
Wanasiasa wanasema uchaguzi huo unaweza kuahirishwa baada ya Saif al-Islam Gaddafi kurejea kwenye kinyang'anyiro cha urais, na Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Abdel Hamid Dabaiba, kukiuka sheria ya uchaguzi na vilevile kutoondolewa Khalifa Haftar kwenye orodha ya wagombea urais, kwa sababu ya tuhuma zinazomkabili za kutenda uhalifu wa kivita.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Serikali ya Libya, Qassem Dabarz, anasema kwamba mgogoro kati ya Khalifa Haftar na Saif al-Islam Gaddafi "ni mzozo kati ya wahalifu wawili wanaotafutwa na mahakama kwa ajili ya uadilifu, na hawatakiwi kushiriki katika medani ya siasa za Libya baada ya kuwanyanyasa wananchi."