Maelfu waandamana Zimbabwe kumuunga mkono Mugabe
Maelfu ya wananchi wa Zimbabwe wamejitokeza barabarani katika mji mkuu Harare, kushiriki maandamano ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 92.
Waandamanaji hao waliokuwa wamevaa fulana zenye picha za rais huyo walikuwa wamebeba mabango na maberamu yenye ujumbe wa kumuunga mkono rais huyo mkongwe ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu. Baadhi ya mabango yalikuwa na ujumbe unaosema "Rafiki yetu Mugabe si mgonjwa, watu wanadanganya kuhusu afya yake". Habari zinasema kuwa, wafuasi wa chama tawala cha rais huyo cha ZANU-PF ambao walikuwa wamebeba bendera ya nchi walisafirishwa kwa mabasi na malori kupelekwa kwenye mji mkuu Harare, baadhi yao wakitokea maeneo ya vijijini kwa ajili ya kushiriki katika maandamano hayo ambayo walioyaandaa wameyapa jina la 'maandamano ya watu milioni moja'. Haya yanajiri huku yakizidi kuongezeka mashinikizo ya ndani ya nje ya nchi ya kumtaka kiongozi huyo aliyeiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 35 aachie madaraka. Mugabe ambaye anapania kuwania urais kwa muhula wa tano na mwisho katika uchaguzi wa mwaka 2018 ambapo atakuwa na miaka 94, hivi karibuni alisema chama tawala cha ZANU-PF ndicho kitaamua mrithi wake na kuonya kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama wanaomshinikiza ajiuzulu. Hii ni katika hali ambayo, Tinomoda Chinoka, wakili wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe ametaka kuchunguzwa hali ya afya ya rais huyo ili kuwa na uhakika kuhusiana na uongozi wake.