Iran yasisitiza kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza azma yake ya kuimarisha uhusiano wa pande zote na bara la Afrika.
Hayo yamedokezwa na Hussein Amir Abdullahian, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran anayshughulikia masuala ya Afrika na nchi za Kiarabu. Akizungumza Jumatano usiku mjini Tehran kwa munasaba wa Siku ya Kimataifa ya Afrika, Abdullahian alisema: "Kuongezeka kiwango cha safari za jumbe za ngazi za juu za Afrika nchini Iran zikiwemo safari za marais wa Ghana na Afrika Kusini mjini Tehran hivi karibuni, ni jambo linaloashiria kuimarika ushirikiano wa Iran na Afrika."
Amongeza kuwa, bara la Afrika ambalo lilipata masaibu makubwa katika zama za ukoloni sasa limechukua mkondo sahihi wa ustawi na kwamba Iran itaendeleza ushirikiano na misaada ya ustawi kwa bara hilo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran aidha ameashiria ugaidi kama jambo chungu ambalo linasumbua baadhi ya maeneo ya Afrika na kubaini kuwa, kuongezeka misimamo mikali na ukosefu wa usalama ni kizingiti katika ustawi wa kibinadamu, kijamii na kiuchumi katika baadhi ya maeneo ya Afrika.