Rais wa Zimbabwe atoa msamaha kwa wafungwa wanawake kupunguza gharama
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametoa msamaha kwa wafungwa wote wanawake ghairi ya waliohukumiwa kifo au kifungo cha maisha huku jela za nchi hiyo zikikabiliwa na tatizo la chakula cha kuhudumia wafungwa kutokana na kukosa fedha kutoka serikalini.
Rais wa Zimbabwe ametoa msamaha kwa wafungwa hao wanawake bila ya kutaja sababu ya kuchukua uamuzi huo na imeripotiwa kuwa wafungwa hao walianza kuachiwa huru jana.
Ripoti zinaeleza kuwa wafungwa watano walifariki dunia mwezi Machi mwaka jana baada ya kupigwa risasi na polisi walipolalamikia uhaba wa chakula uliogeuka kuwa fujo na machafuko na baadhi yao kuitumia fursa hiyo kutaka kutoroka jela.
Msemaji wa Idara ya Huduma za Jela na Urekebishaji wa Tabia nchini Zimbabwe Priscilla Mthembo, amesema kuna jumla ya wafungwa 580 wanawake katika jela zote 46 za nchi hiyo na kwamba wale waliotimiza masharti yaliyokusudiwa wataachiliwa huru.
Kwa mujibu wa Bi Mthembo, kwa ujumla, zaidi ya wafungwa 2,000 watanufaika na msamaha uliotolewa na Rais Mugabe wakiwemo vijana wenye umri mdogo, bila kujali makosa waliyofanya pamoja na wanaume ambao hawatumikii vifungo vya makosa makubwa ya uhalifu kama kuua, wizi wa kutumia silaha, uhaini, ubakaji au kuiba gari kwa kutumia nguvu.
Jela za Zimbabwe zina jumla ya wafungwa 20,000, idadi ambayo ni zaidi ya uwezo wake wa kuchukua wafungwa 17,000 na hivyo kusababisha msongamano na uhaba wa kila kitu katika jela hizo ikiwemo chakula na sare za wafungwa.../