Watu 6 wauawa katika shambulio la al-Shabaab Lamu, Kenya
(last modified Mon, 03 Jan 2022 11:04:51 GMT )
Jan 03, 2022 11:04 UTC
  • Watu 6 wauawa katika shambulio la al-Shabaab Lamu, Kenya

Kwa akali watu sita wameuawa katika shambulio la kundi la kigaidi la al-Shabaab katika kaunti ya Lamu, Pwani ya Kenya.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, wanachama wa al-Shabaab mapema leo Jumatatu wamevamia eneo la Widhu Majembeni katika kaunti ya Lamu, kusini mashariki mwa Kenya, mpakani na Somalia, na kutekeleza ukatili huo.

Akithibitisha tukio hilo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia amesema mmoja wa wahanga wa hujuma hiyo ameuawa kwa kupigwa risasi, mwingine ameuliwa kwa kukatwa kwa mapanga, huku wanne wakiuawa kwa kuchomwa moto wakiwa ndani ya majumba yao.

Magaidi hao wa genge la ukufurishaji la al-Shabaab kadhalika wameteketeza kwa moto nyumba kadhaa za wakazi wa eneo hilo la Widhu Majembeni.

Kambi ya wanajeshi wa Kenya kaunti ya Lamu

Wanachama wa al-Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia katika miji na vijiji vya kaunti ya Lamu kwa miaka mingi sasa, na kisha kwenda kujificha katika msitu wa karibu wa Boni.

Jumapili, Juni 15, 2014, makumi ya wanamgambo wa al-Shabaab walifanya shambulio la kigaidi dhidi ya kijiji cha Mpeketoni kaunti ya Lamu, na kuua takriban watu 50 na kuwachoma moto milki za umma.

Wanachama wa kundi hilo la kigaidi wamekuwa wakitoa madai yasiyo na msingi kuwa wanaishambulia Kenya kwa kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki imetuma wanajeshi wake Somalia.

Tags