Watoto 2 ni kati ya wakimbizi 3 wa Eritrea waliouawa huko Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78936-watoto_2_ni_kati_ya_wakimbizi_3_wa_eritrea_waliouawa_huko_tigray
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, raia watatu wa Eritrea wakiwemo watoto wawili wameuawa katika shambulio la anga lililoilenga kambi ya wakimbizi katika eneo la Tigray lililoathiriwa na mapigano huko kaskazini mwa Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 07, 2022 15:27 UTC
  • Watoto 2 ni kati ya wakimbizi 3 wa Eritrea waliouawa huko Tigray

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, raia watatu wa Eritrea wakiwemo watoto wawili wameuawa katika shambulio la anga lililoilenga kambi ya wakimbizi katika eneo la Tigray lililoathiriwa na mapigano huko kaskazini mwa Ethiopia.

Shambulio la anga la Jumatano iliyopita katika kambi ya wakimbizi ya Mai Aini karibu na mji wa Mai Tsebri huko Tigray limewajeruhi wakimbizi wengine wanne. Hayo yameelezwa kupitia taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa.

Filippo Grandi Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa amesema amesikitishwa sana na vifo vya raia hao watatu wa Eritrea wakiwemo watoto wawili na kwamba wakimbizi hawapasi kulengwa na mashambulizi yoyote. 

Shirika la UNHCR kwa mara nyingine tena limezitolea wito pande zinazozozana huko Tigray kaskazini mwa Ethiopia kuheshimu haki za raia wote, wakiwemo wakimbizi. Hadi sasa si serikali ya Addis Ababa au harakati ya waasi wa TPLF iliyotoa tamko lolote kuhusu kuuliwa raia hao wakiwa kambini. 

Hali ya wakimbizi katika mzozo wa Tigray 

Disemba 30 mwaka jana Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliripoti kuwa, makumi ya raia wameuawa katika mashambulizi ya anga  kusini mwa eneo la Tigray. Umoja wa Mataifa uliyataja mauaji hayo ya raia kuwa mashambulizi makali zaidi kuwahi kuripotiwa tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

Watu wengi pia walijeruhiwa katika mashambulizi hayo.