Rais wa Tunisia avunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama
(last modified Mon, 07 Feb 2022 02:31:21 GMT )
Feb 07, 2022 02:31 UTC
  • Rais wa Tunisia avunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama

Rais Kais Saied wa Tunisia ametangaza habari ya kulivunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama, huku msuguano mkali ukiendelea kushuhudiwa baina yake na mhimili huo wa dola.

Rais Saeid amesema Baraza Kuu la Idara ya Mahakama ni 'kitu kilichopitwa na wakati' huku akiwatuhumu wanachama wa taasisi hiyo huru ya kutathmini utendaji kazi wa majaji wa nchi hiyo kwa ufisadi.

Akizungumza leo Jumapili, Rais wa Tunisia amesema, "katika Baraza hili, vyeo na nyadhifa huuzwa kulingana na uaminifu. Wanachama wanapokea mabilioni ya rushwa."

Kadhalika Rais Kais Saied ameonekana kwa njia ya isiyo ya moja kwa moja akiwaasa wananchi wa Tunisia kuingia mabarabarani kufanya maandamano ya pili ya kulilaani Baraza Kuu la Idara ya Mahakama la nchi hiyo.

Maandamano ya Watunisia wanaopinga hatua za Rais wa nchi hiyo

Uamuzi huu wa Rais wa Tunisia unaonekana kuwa muendelezo wa hatua anazozichukua kwa ajili ya kudhibiti  masuala yote ya nchi. Hatua hizo zimelaaniwa na wapinzani na Muungano wa Wafanyakazi Tunisia (UGTT).

Tunisia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Januari 25 mwaka uliopita 2021. Rais Kais Saied wa nchi hiyo alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha kutwaa udhibiti wa masuala yote ya utendaji nchini humo.