Watanzania 3 wakamatwa DRC wakituhumiwa kuwa wanachama wa ADF
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuwatia mbaroni raia watatu wa Tanzania, kwa tuhuma za kuwa wanachama wa kundi la wanamgambo wa ADF.
Msemaji wa Jeshi la DRC, Kapteni Anthony Mwalushay amesema Watanzania hao wamekamatwa katika operesheni iliyofanyika katika Bonde la Mwalika, eneo la Bashu mjini Beni, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Amesema hii ni mara kwanza kwa jeshi la nchi hiyo kuwakamata raia wa Tanzania wakihusishwa na kundi hilo la wanamgambo linaoendesha harakati za umwagaji damu mashariki mwa DRC.
Amesema Watanzania hao wamekiri kuwa walisajiliwa kujiunga na genge hilo la wapiganaji katika eneo la Butembo, lakini kilichowapeleka DRC ni kazi ya uchimbaji migodi ambayo walikuwa wamefanya kwa muda.
Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.
Hivi sasa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaendesha operesheni za pamoja za kupambana na wanamgambo wa ADF mashariki mwa DRC.