Feb 17, 2022 08:03 UTC
  • Rais Abdelmadjid Tebboune
    Rais Abdelmadjid Tebboune

Rais wa Algeria amesema kuwa Israel na Morocco zinafanya njama ya kuibua hitilafu kati ya Ofisi ya Rais na Jeshi la Algeria na kuzusha fitna nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesema kwamba, Morocco na utawala wa Kizayuni wa Isarael ndio wanaoendesha njama za kuzusha fitina na kueneza habari za uongo nchini Algeria.

Rais Abdelmadjid Tebboune amesema kuwa, Morocco inatumia vyombo vya propaganda kwa ajili ya kusambaza habari za uongo, kutoa pigo kwa umoja wa kitaifa na kulidhalilisha jeshi la Algeria na kwamba Israel inaihami na kuiunga mkono Morocco katika suala hilo.  

Algeria imekuwa mstari wa mbele kupinga hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Morocco ya kuanzisha uhusiano rasmi na wa wazi wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel. Mwishoni mwa mwaka 2020 pia Algeria ilikata uhusiano wake na nchi jirani ya Morocco baada ya Rabat kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel, na kutokana na ujasusi wa Morocco nchini Algeria kwa kutumia programu ya kijasusi ya Israel ya Pegasus. 

Vilevile Algeria iliongoza juhudi za nchi kadhaa za Afrika zilizofanikisha kusimamishwa nafasi ya utawala wa Kizayuni kama mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

Tags