Feb 27, 2022 08:11 UTC
  • Gavana wa Borno Nigeria aonya kuhusu kundi la kigaidi la ISWAP

Gavana wa Jimbo la Borno, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria hivi karibuni alionya kuhusu hatari ya kuenea satwa ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh tawi la Afrika Magharibi (ISWAP).

Gavana Babagana Zulum ametahadharisha kundi hilo la wakufurishaji ambalo limejitenga na kundi jingine la kigaidi la Boko Haram litaibua hatari kubwa ya ugaidi kuliko ile ambayo inashuhudiwa eneo hilo katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.  Amesema hali itakuwa mbaya iwapo serikali haitachukua hatua kali dhidi ya kundi la kigaidi la ISWAP ambalo sasa linapanga mikakati mipya ya kutekeleza hujuma.

Gavana Zulum ametoa tahadhari hiyo hivi karibuni baada ya mkutano wake wa faragha na Rais Muhammadu Buhari mjini Abuja.

Akifafanua kuhusu tishio hilo la ugaidi amesema: "Ongezeko la magaidi wa ISWAP katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo ni la kutia wasiwasi. Hii ni tahadhari ya mapema. Hatupaswi kuruhusu ISWAP kustawi. ISWAP wana uwezo mkubwa, wana kiasi kikubwa cha fedha na pia wana elimu zaidi. Tutafanya kila tuwezalo kuangamiza ISWAP. Kile ambacho Boko Haram wamekuwa wakifanya ni mchezo ukilinganisha na uwezo wa ISWAP."

Magaidi wakufurishaji nchini Nigeria

Kwa miaka 13 sasa, Nigeria imekuwa ikikabiliana na ugaidi wa kundi la Boko Haram hasa katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Taarifa zinasema tokea mwaka 2009 hadi Februari 2022, watu wasiopungua 350,000 wameuawa katika mashambulizi ya Boko Haram huku wengine milioni tatu wakilazimika kuhama makazi yao katika eneo zima la Ziwa Chad.

 

Tags