Hatimaye Maalim Seif atakiwa afike Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kuhojiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8137-hatimaye_maalim_seif_atakiwa_afike_makao_makuu_ya_polisi_zanzibar_kuhojiwa
Baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kuahirisha hatua ya kumhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, hatimaye hatua hiyo sasa imeelekea kutekelezwa, imebainika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 30, 2016 16:26 UTC
  • Hatimaye Maalim Seif atakiwa afike Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kuhojiwa

Baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kuahirisha hatua ya kumhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, hatimaye hatua hiyo sasa imeelekea kutekelezwa, imebainika.

Hii ni kutokana na kile kilichoonekana kuwa ni taarifa rasmi ya wito wa Jeshi hilo visiwani humo, kumtaka Maalim Seif afike katika Ofisi za Makao Makuu ya Polisi, Ziwani mjini Zanzibar kesho Jumanne saa nne asubuhi.

Maalim Seif alithibitisha kupokea barua hiyo leo Jumatatu akiwa njiani kuelekea Dunga Wilaya ya Kati Unguja, akiendelea na ziara yake katika majimbo yote ya Unguja.

“Ni kweli Maalim amepokea taarifa hiyo na ametakiwa afike Ziwani Jumanne saa nne asubuhi”, amesema Salim Bimani, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa CUF.

Hatua hiyo ya sasa imekuja baada ya uamuzi wa Jeshi hilo wa kuahirisha hatua ya wito wa kumhoji Maalim Seif Ijumaa iliyopita.

Barua hiyo ya kuahirisha, na kama ilivyo ya sasa, ni ile iliyosainiwa na DCP Salum Msangi kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar ya tarehe 26 Mei mwaka huu.