HRW: Rwanda inawanyamazisha watumiaji wa YouTube kwa mfumo wa sheria wa ukandamizaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81450-hrw_rwanda_inawanyamazisha_watumiaji_wa_youtube_kwa_mfumo_wa_sheria_wa_ukandamizaji
Viongozi wa upinzani, waandishi wa habari na watoa maoni nchini Rwanda wananyanyaswa na mamlaka za mahakama kwa hotuba na maoni wanayotoa, na hivyo kuzidisha utamaduni wa kutovumilia upinzani. Hayo yameelezwa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 16, 2022 14:12 UTC
  • HRW: Rwanda inawanyamazisha watumiaji wa YouTube kwa mfumo wa sheria wa ukandamizaji

Viongozi wa upinzani, waandishi wa habari na watoa maoni nchini Rwanda wananyanyaswa na mamlaka za mahakama kwa hotuba na maoni wanayotoa, na hivyo kuzidisha utamaduni wa kutovumilia upinzani. Hayo yameelezwa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW).

HRW imesema katika  ripoti yake iliyotolewa leo Jumatano kuwa shirika hilo limefuatilia nyaraka za mahakama, hukumu na hoja za majaji dhidi ya Wanyarwanda kadhaa ambao wameishia gerezani kutokana na "mfumo mbovu wa sheria wa nchi hiyo.'

Watafiti pia wameashiria ukiukaji wa haki ya kujieleza baada ya kuchambua vielelezo vilivyotumwa na maripota kadhaa katika mtandao wa YouTube ambao sasa wamefunguliwa mashtaka. Serikali ya Rwanda hadi sasa imeshawahoji wapinzani 11 katika uwanja huo. 

Lewis Mudge, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katikati mwa Afrika ameiambia televisheni ya al Jazeera kuwa, watu wa Rwanda hawana uhuru wa kubainisha maoni na mitazamo yao kuhusu jambo lolote ambalo litaonekana kuihoji serikali. 

Katika muongo mmoja uliopita, mtandao wa YouTube uliibuka kama chombo cha kuwatangazia wapinzani kuhusu masuala ya taifa baada ya vyombo vya habari na magazeti; ambapo baadaye vituo vya redio vilianza kufuatiliwa kwa karibu na serikali ya Kigali. 

Lewis amesema si vyombo hivyo vya habari tu vinavyofuatiliwa bali hivi sasa pia watumiaji wa mtandao wa YouTube huko Rwanda  wanafuatiliwa na kulengwa mamlaka za serikali. 

Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katikati mwa Afrika amesema, aghalabu ya watu wanaotumia YouTube huko Rwanda wananyamazishwa na kuhukumiwa adhabu kali ambazo zinaweza kuhusishwa  zaidi na hujuma dhidi ya usalama wa taifa.  HRW  imetupia jicho kisa cha mwana YouTube maarufu wa Rwanda, Dieudonne Niyonsenga, anayejulikana pia kama Cyuma Hassan. Kituo chake cha televisheni ya mtandaoni cha Ishema kinafuatiliwa na watazamaji wengi na vipindi vyake huchambua kadhia mbalimbali nyeti na muhimu kuanzia ukiukwaji wa haki za binadamu hadi ufisadi.  

Diuodinne Niyonsenga

Mwezi Novemba mwaka jana Niyonsenga alipatikana na hatia ya  kughushi, kujifanya mwandishi wa habari na kuzuia kazi za umma akiwa nje wakati wa zuio la kukabiliana na maambukizi ya COVID-19  bila kibali halali cha uandishi habari. Maafisa wa Rwanda mwaka juzi wa 2020 walimtia mbaroni Niyonsenga kwa tuhuma za kujifanya mwandishi wa habari na kughushi kadi ya uandishi habari. Hata hivyo mwezi Machi mwaka jana mahakama nchini Rwanda ilimwachia huru lakini baadaye mamlaka ikakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama. Dieudonne Niyonsenga alipandishwa tena kizimbanii na mwezi Novemba alikutwa na hatia na sasa anatumikia kifungo cha miaka saba jela. 

Kwa upande wake Idara ya Mahakama ya Rwanda ilisema kuwa,  Niyosenga alipotosha umma na kufanya uhalifu wa kughushi kwa kujitangaza kama mwandishi wa habari bila kibali.