Tume ya Uchaguzi Libya: Tupo tayari kwa uchaguzi kukiwepo makubaliano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81580-tume_ya_uchaguzi_libya_tupo_tayari_kwa_uchaguzi_kukiwepo_makubaliano
Tume ya Uchaguzi Libya imesema ipo tayari kuendesha zoezi la uchaguzi mara tu makubaliano ya kisiasa yatakapofikiwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 20, 2022 07:42 UTC
  • Tume ya Uchaguzi Libya: Tupo tayari kwa uchaguzi kukiwepo makubaliano

Tume ya Uchaguzi Libya imesema ipo tayari kuendesha zoezi la uchaguzi mara tu makubaliano ya kisiasa yatakapofikiwa.

Hayo yalisemwa jana Jumamosi na Imad al-Sayeh, Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya (HNEC) na kueleza kuwa, iwapo muafaka wa kisiasa utapatikana, basi chombo hicho kimeshajiandaa ipasavyo kwa ajili ya zoezi hilo la kidemokrasia.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umetangaza utayarifu wa kupatanisha mgogoro wa kisiasa nchini Libya baada ya kuibuka serikali mbili hasimu.

Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, njia pekee ya kuiokoa Libya na kutatua mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika ni kufikia mwafaka wa jinsi ya kufanya uchaguzi.

Uchaguzi Libya

Uchaguzi wa rais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 24 mwaka uliopita nchini Libya, uliakhirishwa kwa sababu mbalimbali. 

Miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa maelewano kati ya makundi ya kisiasa ya nchi hiyo kuhusu suala la kutungwa sheria ya uchaguzi na matatizo ya mahakama yanayotokana na malalamiko dhidi ya baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa rais.