Upinzani wakipiga mweleka chama tawala katika uchaguzi mdogo wa Bunge Zimbabwe
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimepata kura nyingi zaidi ya chama tawala katika uchaguzi mdogo wa Bunge uliofanyika Jumamosi ya juzi.
Televisheni ya serikali ya ZBC imetangaza kuwa, chama cha upinzani cha Citizens’ Coalition for Change (CCC) kimezoa maeneobunge 19 kati ya 28 katika uchaguzi huo, huku chama tawala Zimbabwe cha ZANU-PF ambacho kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1980, kikiambulia maeneobunge 9 tu.
Chama hicho cha upinzani kimeanza kupata umaarufu katika maeneo ya mijini, huku chama tawala kikiendelea kujulikana zaidi katika maeneo ya vijijini. ZANU-PF imehifadhi viti vyote vya maeneobunge ilivyovishinda katika uchaguzi wa mwaka 2018.
Licha ya kubwagwa katika uchaguzi huo mdogo wa Bunge, lakini chama hicho tawala kinaendelea kulidhibiti Bunge la nchi hiyo, kwani kilizoa viti 145 kati ya 210 vya maeneobunge ya nchi hiyo katika uchaguzi wa 2018.
Wadadisi wa mambo wanasema matokeo ya uchaguzi huo mdogo muhimu wa Bunge na Serikali za mitaa Zimbabwe uliofanyika Jumamosi unaashiria kuwa uchaguzi mkuu wa mwakani nchini humo utakuwa na ushindani mkubwa.

Uchaguzi huo mdogo mbali na kufanyika katika maeneo bunge 28 ya nchi hiyo, lakini umefanyika pia katika manispaa 122 za serikali za mitaa nchini humo.
Nelson Chamisa, kinara wa chama cha upinzani cha CCC anatazamiwa kuchuana vikali na Rais Emmerson Mnangagwa wa chama tawala ZANU-PF katika uchaguzi ujao wa rais wa 2023.