UN: Huenda Sudan Kusini ikawekewa vikwazo vipya
Umoja wa Mataifa umesema Sudan Kusini ipo katika ncha ya kuwekewa vikwazo vipya na jamii ya kimataifa kutokana na mwendo wa kinyonga wa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka jana.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, Baraza la Usalama la umoja huo linajiandaa kujadiliana karibuni hivi kuhusu uwezekano wa kufufua na hata kuongeza vikwazo dhidi ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kutoaminiana na ukosefu wa ushirikiano vimetawala serikali hiyo changa ya Rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar. Habari zinasema kuwa, ingawa Russia, China na Misri zimetaka kupewa muda zaidi serikali hiyo ili ijiimarishe na kuutafutia ufumbuzi mzozo wa nchi, lakini imearifiwa kuwa Marekani na Uingereza zinashinikiza kuwekewa vikwazo viongozi wa serikali na watu mashuhuri wa nchi hiyo wanaokwamisha mchakato wa amani. Hivi karibuni, Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa amefurahishwa na hatua iliyofikiwa ya mahasimu wawili nchini humo ya kukubali kufanya kazi kwa pamoja na kumaliza mgogoro wa miaka kadhaa wa nchi hiyo, na kusisitiza kuwa viongozi hao na pande zote husika zinapaswa kuongeza juhudi za kuukamilisha mchakato mzima wa kuunda taasisi zote za serikali hiyo ya mpito.
Itakumbukwa kuwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Sudan Kusini ina mawaziri 30 kutoka kwa wafuasi wa Rais Salva Kiir na wa mkuu wa zamani wa waasi, Riek Machar ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais. Riek Machar aliapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini mara baada ya kurejea mjini Juba mwishoni mwa mwezi Aprili.