Walioaga dunia kwa mafuriko Afrika Kusini waongezeka, wafikia 253
Idadi ya watu waliofariki dunia katika jimbo la KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini kutokana na mafuriko yaliyosababisha uharibifu mkubwa, imefikia zaidi ya 250.
Ripoti kutoka katika jimbo hilo zinasema, zaidi ya watu 253 wameripotiwa kufariki dunia hadi jioni ya jana katika mafuriko hayo.
Barabara kuu katika miji ya Durban na Umlazi zimefungwa kutokana na mafuriko. Aidha barabara kuu inayounganisha Durban na Johannesburg ilifungwa kwa muda na kuvuruga shughuli za uchumi. Hali hiyo ilichangiwa na kukatika kwa umeme huku miundombinu ya nchi ambayo imezeeka ikionekana kushindwa kukabiliana na wingi wa maji.
Taarifa zinasema Msikiti wa Banu Hashim katika eneo la Lady Bruce Place umeporomoka kufuatia mafuriko hayo ya Jumatatu usiku.
Kuna ripoti kuwa juhudi za uokoaji zinatatizwa na ukungu huku helikopta zikiendelea kuokoa manusura.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametembelea eneo hilo na kuahidi kutoa misaada.
Ramaphosa ameyataja maafa hayo kuwa ni nguvu ya kimaumbile. Hata hivyo baadhi ya wananchi wamepinga kauli hiyo ya Rais wa Afrika Kusini wakisema kuwa mifereji duni ya maji na nyumba zilizojengwa vibaya katika maeneo ya mabondeni ndiyo sababu ya idadi kubwa ya vifo.
Serikali ya jimbo la KwaZulu-Natal inakadiria kuwa mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa mabilioni ya pesa na katika miundombinu.

Serikali imetoa wito kwa wananchi kuepuka barabara na madaraja yaliyojaa maji na kuhamia maeneo ya juu.
Mafuriko hayo yametokeo huku wanasayansi wakionya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanachochea mvua kubwa kuliko kawaida, Kusini mwa Afrika.