Kiongozi wa upinzani Rwanda aitahadharisha nchi hiyo kuhusu kuwapokea wakimbizi wa Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82986-kiongozi_wa_upinzani_rwanda_aitahadharisha_nchi_hiyo_kuhusu_kuwapokea_wakimbizi_wa_uingereza
Mbunge wa upinzani nchini Rwanda amekosoa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hiyo na Uingereza kuhusu kuwahamishia Rwanda raia wanaotafuta hifadhi huko Uingereza akisema kuwa, hatua hiyo itasababisha matatizo ya bajeti na kuyumbisha jamii kwa muda mrefu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 27, 2022 11:48 UTC
  • Frank Habineza
    Frank Habineza

Mbunge wa upinzani nchini Rwanda amekosoa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hiyo na Uingereza kuhusu kuwahamishia Rwanda raia wanaotafuta hifadhi huko Uingereza akisema kuwa, hatua hiyo itasababisha matatizo ya bajeti na kuyumbisha jamii kwa muda mrefu.

Frank Habineza amekosoa uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kutuma Rwanda wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi. Habineza ni kati ya wanasiasa wachache wanaopaza sauti zao wakikosoa masuala mbalimbali nchini Rwanda. Frank Habineza ambaye ni kiongozi wa  Democratic Green Party ameyataja makubaliano hayo kuwa si ya kibinadamu huku akihoji uhalali wake.

Amesema chama chake kinapinga kikamilifu makubaliano ya aiana hii iwe ni kati ya Rwanda na Denmark, Uingereza au Israel. Amesema hatua ya kuwatuma watu katika nchi ambayo hawakuichagua ni kinyume na haki za binadamu, na hiyo ni sawa na kuwalazimisha waende popote pale, kitu ambacho si cha kibinadamu. 

Frank Habineza ameeleza hayo wiki kadhaa baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza na Rwanda kutangaza kuwa pande mbili zimefikia makubaliano kuhusu masuala ya uhamiaji na maendeleo ya kiuchumi. Makubaliano hayo yatairuhusu Uingereza kutuma nchini Rwanda raia wote watakaoingia Uingereza kinyume cha sheria ambao watapewa makazi katika nchi hiyo ya Kiafrika.  

Wakimbizi wanaoingia UK kinyume cha sheria 

Kufuatia kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaoingia Uingereza kutoka nchi mbalimbali duniani, wakuu wa London wamechukua hatua kali kuzuia wimbi hilo ambapo sasa wanaoingia nchini humo kama wakimbizi watahamishiwa Rwanda katika kipindi chote cha kuchunguzwa mafaili yao. 

Rwanda imekubali wakimbizi kutoka Uingereza wahamishiwe nchini humo baada ya serikali ya Kenya kukataa ombi la London la kupokea wakimbizi hao.