Miili 25 ya wahajiri yapatikana magharibi mwa Libya
Shirika la Kimataifa la Hilali Nyekundu limesema kuwa miili ya wahajiri 25 waliokufa maji siku chache zilizopita wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya imepatikana katika mji wa Zuwara, magharibi mwa Libya.
Al-Khamis Al-Bosaifi, ofisa wa shirika hilo amesema timu za waokoaji na wapiga mbizi zingali zinatafuta miili zaidi katika ufuo wa Bahari ya Mediterranean. Ofisa huyo wa Hilali Nyekundu amesema haijabainika mazingira ya kufa maji wahajiri hao ingawaje baadhi ya duru za habari zimearifu kuwa boti hizo zilizama kwa kushindwa kuhimili mawimbi ya bahari na pia kujaa abiria kupita kiasi.
Juma lililopita, Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya, kusini mwa Italia. Habari ziliarifu kuwa, aghalabu ya wahajiri waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni raia wa nchi za Kiafika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri.
Wakimbizi karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku mamia ya wengine wakifariki dunia kwa kuzama baharini.