Mamia wauawa katika mashambulizi nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8389-mamia_wauawa_katika_mashambulizi_nchini_libya
Wanajeshi wawili wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wameuawa na wengine 12 kujeruhiwa katika shambulizi la kujitoa mhanga lililofanywa na wanamgambo wa kundi la ISIS (Daesh) karibu na mji wa Sirte hapo jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2016 09:43 UTC
  • Mamia wauawa katika mashambulizi  nchini Libya

Wanajeshi wawili wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wameuawa na wengine 12 kujeruhiwa katika shambulizi la kujitoa mhanga lililofanywa na wanamgambo wa kundi la ISIS (Daesh) karibu na mji wa Sirte hapo jana.

Serikali ya Libya imesema shambulizi hilo limetokea wakati vikosi vya usalama vikielekea mji wa Sirte. Mapigano kati ya vikosi vya usalama na wapiganaji wa kundi la ISIS katika mji wa magharibi wa Sirte Jumatano wiki hii yalisababisha vifo vya askari 10 na wengine 40 kujeruhiwa.

Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu 200 na kujeruhi 300 kutoka pande zote za jeshi la serikali na wanamgambo wa Daesh tangu mwanzoni mwa mwezi Mei.

Hayo yanajiri baada ya vikosi maalumu vya kulinda taasisi za mafuta nchini Libya kulikomboa eneo moja la kiistratijia mashariki mwa mji wa bandari wa Sirte wa kaskazini mwa nchi hiyo, kutoka mikono mwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Msemaji wa vikosi hivyo maalumu amesema kuwa, mji wa Bin Jawwād wa mashariki mwa bandari ya Sirte ambayo ni ngome ya kundi la kigaidi la Daesh, umekombolewa.

Kundi la Daesh lilitumia mwanya wa kukosekana serikali yenye nguvu nchini Libya, kuuvamia na kuuteka mji wa bandari wa Sirte na kupanua eneo la kilomita 250 la udhibiti wake.