Jun 03, 2016 14:46 UTC
  • Kuendelea hali tete Burundi licha ya makataa yaliyotolewa na Nkurunziza

Hali imeendelea kuwa tete nchini Burundi licha ya Rais Pierre Nkurunzinza kutoa muda maalumu kwa kundi la wapinzani wa serikali, wa kuachana na upinzani wao.

Pierre Nkurunziza ametoa muda wa siku 15 kwa waasi wa eneo la Mugamba la kusini magharibi mwa Burundi wabadilishe misimamo yao na warejee jijini Bujumbura, la sivyo serikali itachukua hatua kali dhidi yao. Duru za kiusalama zimetangaza habari ya kuzuka kundi jipya la wapinzani wa hatua ya Pierre Nkurunziza ya kuendelea kubakia madarakani na wamefanya mashambulizi kadhaa katika maeneo ya viunga vya Bujumbura. Kundi hilo la Mugamba lina makao yake katika eneo lililoko umbali wa kilomita 80 kutoka Bujumbura. Kwa mtazamo wa wachambuzi wa mambo, hatua ya serikali ya Burundi ya kuwapa muda wa siku 15 waasi wa eneo la Mugamba wa kuhakikisha wanaacha uasi, ni aina fulani ya juhudi za kujiimarisha Pierre Nkurunziza na kutafuta uungaji mkono wa wananchi sambamba na kujionesha yuko imara katika upeo wa kieneo na kimataifa lakini pia unaweza kuwa mtihani mgumu kwake. Hii ni kwa sababu kama waasi hao wataachana na uasi wao na kurejea jijini bujumbura katika kipindi cha siku 15 zijazo kama inavyotaka serikali, nafasi ya Nkurunziza kati ya wananchi, kieneo na kimataifa itakuwa nzuri. Lakini kama waasi watadharau muda huo uliotolewa na serikali na Pierre Nkurunziza akashindwa kuchukua hatua zozote za kumaliza uasi huo, nafasi ya Rais huyo wa Burundi itadhoofika mbele ya wananchi, na nafasi ya wapinzani itapata nguvu. Hii ni katika hali ambavyo viongozi wa chama tawala cha CNDD-FDD wanamuunga mkono Nkurunziza aendelee kubakia madarakani. Kwa muda wa mwaka mzima sasa chama hicho, serikali ya Burundi na viongozi wake, wanatuhumiwa kufanya ukandamizaji mkubwa wa umwagaji wa damu dhidi ya wapinzani katika kona mbalimbali za Burundi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanalituhumu moja kwa moja tawi la vijana la chama tawala cha CNDD-FDD kuwa ndio wanaohusika na mauaji ya wapinzani. Kama ambavyo imedhihirika wazi kuwa wapiganiaji wa demokrasia nchini Burundi nao wamekatishwa tamaa na suala la kulindwa demokrasia kwa njia za amani na usalama. Kuzuka kundi jipya la waasi wa Mugamba wanaoripotiwa kutumia nguvu kuonesha upinzani wao, ni ushahidi wa waziwazi wa jambo hilo. Wachambuzi hao wanasema kuwa, hakuna dalili zozote za kukatika upinzani dhidi ya hatua ya Rais Nkurunziza ya kuendelea kubakia madaraka kwa vipindi vitatu mfululizo, na ni wazi kuwa upinzani huo utaendelea hadi mwaka 2022 wakati wa uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo wapinzani wa Nkurunzinza wanaonesha kivitendo kuwa hawako tayari kumwacha rais huyo atawale kwa utulivu na amani hadi mwaka 2022. Aidha baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema, ni vigumu kutasawari kwamba waasi wa Mugamba wataitikia mwito wa serikali wa kuhakikisha wanarejea Bujumbura katika kipindi cha siku 15 zijazo, na kama watakataa, basi tutarajie kushuhudia hali tete zaidi nchini Burundi. Hivi sasa rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa aliyeteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi anafanya juhudi za kuzungumza na pande zote husika. Lililobakia kwa sasa ni kusubiri na kuona, je, juhudi hizo za mpatanishi wa Burundi zitawavuta wapinzani kwenye meza ya mazungumzo, au moto wa upinzani utaongezeka katika nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika?

Tags