Polisi Tunisia wapambana na waandamamaji wanaopinga kura ya maoni ya Julai
Mapambano yamezuka mjini Tunis kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga kura ya maoni iliyoitishwa na Rais Kais Saeid wa Tunisia kufanyika nchini humo mwezi ujao wa Julai takriban mwaka mmoja tangu kiongozi huyo alipochukua hatua inayoelezewa na wakosoaji wake kama mapinduzi ya kijeshi.
Askari polisi jana waliwazuia waandamanaji waliokuwa wakielekea makao makuu ya tume ya uchaguzi ambayo mkuu wake alibadilishwa na Rais Saeid na kushika uongozi wake yeye mwenyewe katika hatua inayolenga kupanua wigo wa udhibiti wake kwa taasisi za dola.
Katika maandamano hayo yaliyoandaliwa na vyama vidogo vitano vya siasa, baadhi ya waandamanaji walibeba mabango yaliyoandikwa: "Tume ya rais ni sawasawa na tume ya udanganyifu."
Julai 25, 2021, Rais Kais Saeid wa Tunisia alivunja serikali na kulisimamisha bunge, ambalo nalo pia alilivunja hatimaye, hatua ambazo zilizusha hofu ya kutoweka demokrasia pekee iliyoibuka kutokana na vuguvugu la kinachojulikana kama Machipuo ya Kiarabu.
Rais wa Tunisia amepanga kuitisha kura ya maoni ya rasimu ya katiba mnamo mwezi ujao itakayochukua nafasi ya katiba ya mwaka 2014 yenye mfumo mseto wa bunge na urais.
Siku ya Jumatano kiongozi huyo aliwafuta kazi pia majaji 57 akiwatuhumu kwa ufisadi na kuwalinda wale aliowaita magaidi.
Majaji waliofukuzwa wamesema, hatua iliyochukuliwa dhidi yao imetokana na msimamo wao wa kupinga uingiliaji wa kazi zao unaofanywa na waziri wa sheria na wa watu waliomzunguka rais.
Majaji nchini Tunisia walitangaza jana kuwa wanapanga kusita kufanya kazi mahakamani kwa muda wa juma zima na kuendesha mgomo wa kuketi kulalamikia kutimuliwa majaji wenzao.../