Zaidi ya 130 wauawa katika mashambulizi ya magaidi nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i84976-zaidi_ya_130_wauawa_katika_mashambulizi_ya_magaidi_nchini_mali
Makumi ya raia wameuawa nchini Mali katika wimbi jipya la magenge ya wanamgambo wanaobeba silaha katikati ya nchi hiyo ya eneo la Sahel.
(last modified 2026-01-05T08:06:51+00:00 )
Jun 21, 2022 07:48 UTC
  • Zaidi ya 130 wauawa katika mashambulizi ya magaidi nchini Mali

Makumi ya raia wameuawa nchini Mali katika wimbi jipya la magenge ya wanamgambo wanaobeba silaha katikati ya nchi hiyo ya eneo la Sahel.

Maafisa wa serikali katika eneo hilo wamesema magenge ya wabeba silaha mwishoni mwa wiki yaliwashambulia wanavijiji katika eneo la Diallassagou na vile vile miji miwili katika eneo la Bankass, na kuua zaidi ya watu 130.

Afisa mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake kutokana na sababu za kiusalama amesema, "mbali na mauaji, wavamizi wamechoma moto nyumba na kuiba mifugo. Idadi kamili ya waliouawa haijajulikana, kwa kuwa hadi (jana) Jumatatu maiti zilikuwa zinaendelea kupatikana."

Naye Nouhoum Togo, kiongozi wa chama kimoja cha siasa katika eneo la Bankass katikati ya Mali amesema idadi ya waliouawa ni kubwa ikilinganishwa na idadi iliyotangazwa na serikali ya 132, na kwamba wanaosadikika kuhusika na hujuma hizo ni wachama wenye mfungamano na genge la al-Qaeda. 

Hii ni katika hali ambayo, kwa akali watu wanane waliuawa katika shambulizi jingine la kigaidi lililotokea katika jiji la Koutiala kusini mwa Mali wiki iliyopita.

Magaidi wanaotishia usalama wa eneo la Sahel

Magaidi wa makundi ya ukufurishaji yanayofungamana na ISIS au al-Qaeda wamekuwa wakitekeleza mashambulizi dhidi ya raia na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu sasa katika nchi ya Mali na nchi nyingine za eneo la Ziwa Chad, magharibi mwa Afrika.

Mgogoro wa hali mbaya ya kiusalama umeigubika Mali tangu mwaka 2012; na vikosi vya majeshi kutoka nje hasa vya Ufaransa vilivyotimuliwa hivi karibuni havijaweza kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo.