EAC yataka waasi wa M23 waondoke mara moja mashariki mwa DRC
(last modified Tue, 21 Jun 2022 08:02:14 GMT )
Jun 21, 2022 08:02 UTC
  • EAC yataka waasi wa M23 waondoke mara moja mashariki mwa DRC

Jumuiya ya Afrika Mashariki imelitaka kundi la waasi la M23 liondoke mara moja katika mji wa Bunagana unaodhibitiwa na wanamgambo hao, huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aidha viongozi wa EAC wameafikiana juu ya kutekelezwa kivitendo mpango wa kutumwa wanajeshi wa kieneo katika eneo la mashariki mwa Kongo DR kwenda kukabiliana na magenge ya waasi.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana Jumatatu aliongoza mkutano wa marais sita wa nchi wanachama wa EAC katika Ikulu ya Nairobi, ambapo moja ya ajenda kuu za kikao hicho ni mzozo baina ya Rwanda na DRC. 

Mbali na Kenyatta, viongozi wengine wa EAC walioshiriki mkutano wa jana ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Felix Tshisekedi wa DRC, Évariste Ndayishimiye wa Burundi, Paul Kagame wa Rwanda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, huku Tanzania ikiwakilishwa na John Steven Simbachawene, Balozi wa nchi hiyo jijini Nairobi. 

Waasi wa M23

Kongo DR imekuwa ikisisitiza kwamba, Rwanda inaunga mkono waasi wa M23 ambao wanalaumiwa kwa mashambulio nchini humo. Rwanda imekanusha vikali madai hayo, na yenyewe ikiituhumu DRC kuwa inawaunga mkono waasi walio dhidi ya serikali ya Kigali.

Kabla ya kufanyika mkutano huo wa jana jijini Nairobi, DRC kupitia msemaji wake, Patrick Muyaya ilitangaza kuwa imeafiki askari wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki watumwe mashariki mwa nchi hiyo kukabiliana na waasi, kwa sharti kuwa wanajeshi wa Rwanda wasiwe katika kikosi hicho. Radio Tehran haijaweza kubaini iwapo askari wa Rwanda watajumuishwa kwenye kikosi hicho au la.

 

Tags