Watu 18 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani Pwani ya Kenya
Watu 18 wamepoteza maisha huku wengine wengi wakijeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha gari dogo la abiria na lori katika kaunti ya Kwale, Pwani ya Kenya.
Kamanda Mkuu wa Polisi katika kaunti ya Pwani, Titus Karuri amethibitisha habari ya kutokea ajali hiyo na kueleza kuwa, watoto wawili ni miongoni mwa watu 18 walioaga dunia kwenye ajali hiyo ya jana jioni.
Habari zinasema kuwa, matatu hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 18 iligongana na trela katika eneo lililoko baina ya Taru na Samburu, katika barabara kuu ya Nairobi kwenda Mombasa.
Mashuhuda wanasema gari hilo dogo la abiria lilikuwa linaendeshwa kwa kasi, na lililogongana ana kwa ana na lori lililokuwa likitokea upande wa pili, lilipojaribu kulipita gari jingine.
Miili ya wahanga wa ajali hiyo imepelekwa katika Makafani ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kinago, kaunti ya Kwale, Pwani ya Kenya.
Kwa wastani, Wakenya 3,000 hupoteza maisha kila mwaka katika ajali za barabarani. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa, duniani kote ajali za barabarani zinaua watu takriban milioni 1.3 kila mwaka ambao ni sawa na zaidi ya watu wawili kila dakika, huku wengine milioni 50 wakijeruhiwa.