Jul 26, 2022 06:33 UTC
  • Safari ya Lavrov barani Afrika; juhudi za Russia za kutafuta fursa mpya

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameanza safari yake ya siku 5 barani Afrika kwa kuitembelea Misri ambako aliwasili Jumapili, Julai 24.

Akiwa Misri amekutana na Rais Abdelfattah El-Sisi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sameh Shoukry. Lavrov pia amepangiwa kuzitembela nchi za Ethiopia, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo atakutana na kuzungumza na viongozi wa nchi hizo. Hata kama Lavrov amejadiliana masuala mbalimbali na viongozi wa Misri katika safari yake hiyo lakini la muhimu zaidi ni kuwa pande mbili zimejadili njia za kupunguza matatizo yanayoikabili Misri kwa sasa katika kujidhaminia chakula kutoka Russia kwa kutilia maanana kuwa nchi hiyo ya Kiarabu inapitia matatizo mengi katika uwanja huo kwa kuzingatia kuwa huagiza sehemu kubwa ya chakula chake na hasa ngano kutoka Russia na Ukraine, suala ambalo limevurugwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Moscow imekuwa ikizilaumu mara kwa mara nchi za Magharibi kwa kuzuia mauzo ya ngano na bidhaa nyingine za kimkakati kutoka Russia. Katika muktadha huo, huku akionyesha matumaini ya kufanikiwa makubaliano ya mauzo ya nafaka yaliyotiwa saini karibuni mjini Istanbul, Lavrov amesisitiza kuwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Russia vimezuia usafirishaji wa nafaka na meli za mizigo kutoka nchi hiyo. Amesema: "Moscow inatumai kuwa Umoja wa Mataifa, ukiwa sehemu muhimu ya "makubaliano ya chakula", utaweza kuondoa vikwazo haramu vinavyozuia usafirishaji wa nafaka kutoka Russia." Wakati huo huo, ukweli kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameichagua Misri kuwa kituo cha kwanza cha safari yake barani Afrika unaonyesha umuhimu wa nchi hiyo katika mipango ya Moscow na pia ni njia ya kutoa shukrani kwa msimamo wa Misri kuhusu vita vya Ukraine.

Vita vya Ukraine vimetatiza pakubwa uagizai wa ngano kutoka nchi hiyo

 

"Hussein Haridi", Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri na mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa, katika kuchambua safari ya Lavrov, anasema: Cairo ni moja ya vituo muhimu vya safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia barani Afrika, kwa kuzingatia hali tata ya hivi sasa katika upeo wa kimataifa. Safari ya Lavrov mjini Cairo imefanyika katika fremu ya uhusiano wa kimkakati kati ya Misri na Russia kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, kutokana na msimamo wa busara wa Misri wa kutoegemea upande wowote katika vita vya Russia na Ukraine.

Suala muhimu linalojitokeza wazi katika safari ya mara hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia katika nchi za Kiafrika ni jaribio la Moscow la kujiondoa katika hali ya kutengwa kisiasa kimataifa kwa kuongeza maingiliano ya kisiasa na kidiplomasia na nchi za Afrika, na pia kutafuta barani humo fursa mpya za kiuchumi na kibiashara. Tangu kuanza vita vya Ukraine, nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zimetekeleza vikwazo vikali zaidi dhidi ya Russia katika nyanja zote zinazowezekana, na hilo limeisababishia nchi hiyo matatizo mengi.

Katika hali hiyo, ni kawaida kwa Russia kutafuta washirika wapya wa kisiasa, kibiashara na kiuchumi na kuelekeza juhudi zake katika kupanua uhusiano na nchi ambazo hazijaunga mkono msimamo wa Magharibi katika kuiwekea vikwazo Russia, bali zinataka kudumisha na hata kupanua mahusiano na Moscow katika nyanja tofauti.

Juhudi za sasa za Moscow zinaonekana kulenga katika kupanua uhusiano wa kisiasa na nchi za Kiafrika. Kuhusiana na hilo, siku tatu zilizopita,  na akizungumza katika mkutano na waandishi habari, kabla ya kuanza safari yake katika nchi kadhaa za Afrika, Lavrov alisema kuwa safari hii imejikita katika maandalizi mazuri ya mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na Russia, ambao mahali pa kufanyika kwake patatangazwa baadaye. Kabla ya hapo Lavrov alikuwa ametangaza kwamba mkutano ujao kati ya Russia na Afrika utafanyika katika mojawapo ya nchi za Kiafrika mnamo 2022.

Serikali ya Rais El-Sisi imejizuia kuilaumu Russia kuhusu vita vya Ukraine

Viongozi wa Moscow wamesisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuwa na uhusiano mzuri na nchi za Afrika. Kuhusiana na hilo, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa ushirikiano na nchi za Afrika ni wa kimkakati na wa muda mrefu, na kwamba kuendeleza uhusiano na nchi za Afrika na mashirika ya kikanda ya bara hilo ni moja ya vipaumbele vya sera ya nje ya Russia. Theodore Murphy  Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Ulaya, anasema: Russia kwa mara nyingine tena imepata fursa ya kurejesha ushawishi wake barani Afrika kwa kutoa misaada ya usalama yenye masharti machache kuliko nchi za Magharibi na pia kuzisaidia kisiasa nchi hizo kinyume na zinavyofanya nchi za Magharibi ambazo daima hukosoa na kuzikemea nchi za Kiafrika.

 

Tags