Afrika yalilia chanjo ya Monkeypox iliyoua watu 75 barani humo
Afrika haina hata dozi moja ya chanjo ya kupambana na ugonjwa wa Ndui ya Nyani (Monkeypox), licha ya kuwa bara pekee lililosajili vifo vilivyotokana na maradhi hayo.
Kaimu Mkuu wa Kituo cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa Afrika (Africa CDC), Ahmed Ogwell amesema kama ilivyoshuhudiwa wakati wa janga la Corona, bara Afrika kwa mara nyingine limetengwa na kukosa chanjo za Homa ya Nyani.
Ogwell amesisitizia haja ya kupelekwa chanjo za kukabili maradhi hayo katika bara hilo lenye watu zaidi ya bilioni 1.3, ili kuzuia maafa zaidi.
Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya kesi 20,000 za ugonjwa huo zimeripotiwa katika nchi 78 duniani katika mripuko huu mpya, nyingi zikiwa barani Ulaya.
Afrika CDC imesema kufikia sasa kesi 2,101 za maradhi hayo zimeripotiwa barani Afrika, mbali na vifo 75 tangu mwanzoni mwaka huu 2022. Hata hivyo taasisi hiyo ya Umoja wa Afrika imesema kesi zilizothibitishwa hadi sasa barani humo ni 283, huku kesi 1,818 zikishukiwa kuwa za ugonjwa huo.

Siku chache zilizopita Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza ugonjwa wa Ndui ya Nyani (Monkeypox) kuwa tishio la afya duniani.
Utafiti unaonesha kuwa, maambukizi ya ugonjwa huo yanaongezeka, huku asilimia 95 ya walioambukizwa wakiwa ni wanaume wanaoshiriki ngono ya jinsia moja.