Burundi yatuma wanajeshi DRC kufuatia uamuzi wa EAC
(last modified Wed, 17 Aug 2022 12:13:16 GMT )
Aug 17, 2022 12:13 UTC
  • Burundi yatuma wanajeshi DRC kufuatia uamuzi wa EAC

Burundi imekuwa nchi ya kwanza kutuma wanajeshi wake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia uamuzi wa karibuni hivi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa kutuma kikosi cha pamoja cha kieneo katika nchi hiyo ili kwenda kupambana na magenge ya waasi na wanamgambo.

Kwa mujibu wa Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  (FARDC), kikosi hicho cha askari wa Burundi kilichowasili nchini humo juzi Agosti 15 kitatumwa katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa DRC kwenda kukabiliana na magenge ya waasi wanaobeba silaha.

Jeshi la Kongo DR limesema askari hao wa Burundi wametumwa nchini humo katika fremu vikosi vya pamoja, mpango ambao uliafikiwa karibuni hivi na viongozi wa jumuiya ya EAC, chini ya uenyekiti wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Habari zaidi zinasema kuwa, wanajeshi hao wa Burundi watakita kambi katika kituo cha mafunzo cha Luberezi, yapata kiloita 100 kutoka Bukavu, mji mkubwa zaidi katika mkoa wa Kivu Kusini.

Katika mkoa huu, kundi la wabeba silaha la Mai-Mai kwa upande mmoja, na magenge ya Twirwaneho na Gumino kwa upande wa pili yamekuwa yakikabiliana na kupigana kila uchao.

Magenge ya waasi DRC

Luteni Marc Elonga, Msemaji wa Jeshi katika mkoa wa Kivu Kusini amewataka wakazi wa eneo hilo kuwa watulivu na kushirikiana na kikosi hicho cha Burundi ambacho kitakuwa chini ya kamandi ya DRC, ili waweze kuzima harakati za magenge ya waasi na wapiganaji wanaobeba silaha na kuhatarisha usalama wa raia na maafisa usalama mashariki ya Kongo DR.

Novemba mwaka jana, DRC na Uganda zilizindua operesheni za pamoja dhidi ya wanamgambo wa ADF, waliojificha katika misitu ya mashariki ya Kongo DR. 

 

Tags