50,000 watoroka Niger kufuatia hujuma za magaidi wa Boko Haram
(last modified Wed, 08 Jun 2016 03:38:54 GMT )
Jun 08, 2016 03:38 UTC
  • 50,000 watoroka Niger kufuatia hujuma za magaidi wa Boko Haram

Melfu ya watu wamekimbia nyumba zao kusini kaskazini mwa Niger kufuatia mfululizo wa mashambulizi toka kwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram walioko mjini Bosso mkoani Diffa.

Mashambulizi hayo yalijiri Ijumaa, Jumapili na Jumatatu na hadi hii leo hali mjini Bosso bado ni tata. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR lilionya mapema mwezi uliopita kwamba hali ya usalama katika mkoa huo ni mbaya na kwamba shirika hilo halijaweza kuhudumia moja kwa moja eneo hilo tangu Feberuari mwaka jana, wapiganaji wa Boko Haram walipoingia kutoka Nigeria.

Shirika hilo limesema limekuwa likitoa msaada katika eneo hilo kupitia wadau wa mashinani na kwamba timu ya dharura inatarajiwa kuweka kambi mkoani Diffa juma hili. Adrian Edwards msemaji wa UNHCR amesema, ''machafuko yalienea kote mkoani Bosso mwezi Mei yakiwemo mauaji ya Mei 31 karibu na mji wa Yebi yaliyoacha watu tisa wakiwa wamefariki na kulazimisha wakazi karibu 50,000 na wakimbizi wa ndani kusaka malazi Bosso.''

Juzi wananchi wa mji mkuu wa Niger, walifanya maandamano makubwa ya kutangaza uungaji mkono wao kwa wahanga wa mashambulizi ya hivi karibuni ya genge la kigaidi la Boko Haram.

Katika shambulio la karibu kabisa la siku ya Ijumaa, magaidi wakufurishaji wa Boko Haram walivamia kambi ya kijeshi ya Niger katika eneo la mpakani la Bosso la kusini mashariki mwa nchi hiyo na kuua wanajeshi 30 wa Niger na wanajeshi wawili wa Nigeria na kujeruhi wengine 67.

Tags