Aug 24, 2022 08:01 UTC
  • Wananchi wa Angola leo wanamchagua Rais; upinzani watishia kupinga matokeo

Wananchi wa Angola waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanashiriki katika uchaguzi kwa ajili ya kumchagua rais mpya wa nchi hiyo.

Zaidi ya Waangola milioni 14 wamejiandikisha kama wapiga kura na watamchagua rais na Wabunge 220 kwa wakati mmoja, kwa kuweka alama moja kwenye karatasi ya kupigia kura.

 Uchaguzi huo umetajwa kuwa na ushindani wa aina yake na mkali kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa vuguvugu la siasa za vyama vingi mwaka 1992 nchini Angola

Rais aliyeko madarakani    João Lourenço,  anayewania muuhula wa pili anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha upinzani cha UNITA Adalberto Costa Junior.

Chama tawala cha Peoples Movement for the Liberation of Angola – MPLA, kimetawala Angola tangu nchi hiyo ijipatie uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

Chama kikuu cha upinzani cha The National Union for the Total Independence of Angola UNITA, kimepata umaarufu mkubwa sana nchini humo kinyume na ilivyokuwa katika uchaguzi wa awali.

Tayari chama cha upinzani cha UNITA kimeituhumu serikali kwa kujaribu kulazimisha utawala wa chama kimoja, na kwamba kinafikiria kupinga matokeo ya uchaguzi, ambao chama hicho kinaona kwamba huenda usiendeshwe kwa njia ya haki na ya huru.

Kiongozi wa chama hicho Adalberto Costa Junior amesema kwamba, utawala wa MPLA, hautaki kabisa Angola kuwa nchi yenye demokrasia.

Angola, ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta Afrika, ilikumbana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa muda wa miaka 27.

Tags