Kushadidi mgogoro nchini Libya kwa kuanza tena vita na mapigano makali
(last modified Mon, 29 Aug 2022 13:11:20 GMT )
Aug 29, 2022 13:11 UTC
  • Kushadidi mgogoro nchini Libya kwa kuanza tena vita na mapigano makali

Kufuatia kushadidi mzozo wa kisiasa nchini Libya kati ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Abdul Hamid al-Dbeibeh na serikali mpya iliyopewa mamlaka na Bunge inayoongozwa na Fathi Bashagha, mapigano yameanza upya kati ya vikosi vya pande hizo mbili katika mji mkuu Tripoli.

Hadi sasa watu wasiopungua 23 wameuawa na kwa akali 87 wamejeruhiwa.

Mgogoro wa kisiasa nchini Libya umepamba moto katika miezi ya hivi karibuni. Kuteuliwa Fathi Bashagha kuwa Waziri Mkuu mpya wa Libya na Baraza la Wawakilishi lenye makao yake makuu mjini Tobruk mnamo mwezi Februari mwaka huu kumevuruga hali ya kisiasa ya nchi hiyo na kuifanya iwe mbaya tena.

Libya ilishuhudia utulivu wa kiwango fulani baada ya usitishaji vita uliofikiwa mwaka 2020 na kufuatiwa na uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa mwanzoni mwa mwaka 2021. Sambamba na hayo, mazungumzo ya kutafuta suluhu na juhudi za kuitisha uchaguzi mkuu utakaoshirikisha makundi na mirengo tofauti ya nchi hiyo, zikawa zinaendelea kufanywa. Lakini kuchaguliwa Fathi Bashagha kuwa waziri mkuu, mtu ambaye anaungwa mkono na Jenerali Khalifa Haftar kumeitibua tena hali ya mambo katika nchi hiyo.

Abdul Hamid al-Dbeibeh

 

Bashagha anajitambua kuwa ndiye waziri mkuu halali wa Libya kwa sasa; na ameitaka serikali ya Umoja wa Kitaifa ifunge virago na kukabidhi kwake yeye hatamu za madaraka. Hata hivyo, waziri mkuu wa serikali hiyo Abdul Hamid al-Dbeibeh ansisitiza kuwa hatakabidhi madaraka isipokuwa kwa serikali itakayochaguliwa na wananchi kupitia uchaguzi wa rais na wa wabunge.

Kutokana na upinzani ulioonyeshwa na serikali ya umoja wa kitaifa, Fathi Bashagha ametishia kuwa atatumia mtutu wa bunduki kuuteka mji mkuu Tripoli na kuhitimisha udhibiti wa serikali ya umoja wa kitaifa kwa mji huo.

Hali hiyo ndiyo iliyosababisha kuwaka tena moto wa vita nchini Libya. Mapigano makali yameshuhudiwa katika muda wa siku mbili zilizopita kati ya vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa na wapiganaji watiifu kwa Fathi Bashagha.

Fathi Bashagha

 

Hadi hivi sasa mapigano yanaendelea na hali imeripotiwa kuwa mbaya sana katika baadhi ya maeneo ya Tripoli. Hayo yanajiri huku wizara ya mambo ya ndani ya serikali ya Bashagha ikisisitiza kuwa, haitanyamazia kimya katu matukio na mapigano hayo na kwamba itachukua kila hatua inayohitajika kwa ajili ya kuwalinda raia na taasisi za serikali katika mji mkuu huo wa Libya. 

Abdul Hamid al-Dbeibeh, waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa, yeye ameendelea kutilia mkazo dai lake la kufanyika uchaguzi.

Kuhusiana na nukta hiyo na yanayoendelea kujiri nchini Libya, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa na amani, Bi Rosemary DiCarlo ameema: "tunaamini kwa dhati kabisa kuwa, uchaguzi ndio njia pekee ya kutatua tofauti juu ya uhalali wa kidemokrasia wa taasisi zote za Libya."

Mapigano ya hivi karibuni baina ya makundi yanayobeba silaha katika mji mkuu Tripoli yanadhihirisha mpasuko mkubwa uliopo kati ya miungano miwili mikuu ya kijeshi na kisiasa ya nchini humo. Vita kamili vinavyohofiwa kutokea kwa ajili ya kudhibiti mji huo vinaweza kwa kiwango kikubwa vikawa tofauti kabisa na vile vilivyoshuhudiwa katika mwaka 2019 na 2020.

Rosemary DiCarlo

 

Kwa upande mwingine, mapigano yanayoendelea hivi sasa yanatoa mwanya kwa uingiliaji wa maajinabi na madola ya kigeni nchini Libya. Wakati Vita vya Ukraine vimeathiri soko la kimataifa la mafuta na gesi, sasa hivi nchi za Magharibi zimeshapata tena fursa mwafaka ya kushadidisha mgogoro wa ndani ya Libya ili kuandaa mazingira ya kujineemesha kwa kupora maliasili za nchi hiyo. Abdul Hamid al-Dbeibeh, waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa  anasema: "mapigano ya Tripoli yamepangwa na kuratibiwa kutokea ndani na nje ya nchi hii."

Ikiwa vita vitaendelea, maliasili za Libya zitazidi kukabiliwa na hatari ya kunyonywa na kuporwa; na uwezekano wa nchi hiyo kugawanyika na kushamiri ndani yake makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka utazidi kuwa mkubwa. Kwa hiyo, kama walivyowahi kusisitiza mara kadhaa viongozi wenyewe wa nchi hiyo, huenda kuitishwa uchaguzi ukawa ndio mwarubaini wa kuinasua Libya kwenye mgogoro ambao ulianza kwa uingiliaji wa madola ya kigeni na umekuwa ukiendelea kwa uingiliaji wa madola hayo pia.../