Makumi ya maiti zagunduliwa katika kaburi la umati Sirte, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i88836
Mamlaka ya Libya imetangaza kupatikana kwa miili 42 ambayo haikutambuliwa katika kaburi la pamoja huko Sirte, makao makuu ya zamani ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 03, 2022 07:43 UTC
  • Makumi ya maiti zagunduliwa katika kaburi la umati Sirte, Libya

Mamlaka ya Libya imetangaza kupatikana kwa miili 42 ambayo haikutambuliwa katika kaburi la pamoja huko Sirte, makao makuu ya zamani ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).

Kundi la kigaidi la ISIS lilikuwa limeufanya mji wa Sirte nchini Libya kuwa makao yake makuu kati ya 2015-2016.

Magaidi wa kundi hilo waliulinda vikali mji huo kwa kutumia mbinu za msituni lakini mwishoni mwa 2016, walishindwa na vikosi vya jeshi vinavyounga mkono serikali.

Mamlaka ya Libya ilitangaza jana Jumapili kwamba miili hiyo ya watu 42 iligunduliwa huko Sirte, makao makuu ya zamani ya kundi la ISIS, kilomita 450 mashariki mwa Tripoli, na kwamba wameanza kuchukua sampuli za mifupa ya miili hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).

Mnamo Oktoba 2017, miili 21 ya Wakristo wa Kicopti waliouawa na Daesh mwaka 2015 iligunduliwa pia kwenye kaburi la pamoja karibu na mji huo wa Sirte.

Hivi majuzi, mwishoni mwa mwezi Agosti pia, makaburi mawili ya halaiki yenye miili saba na minane, mtawalia, yaligunduliwa katika yadi ya hospitali huko Sirte.

Tangu kupinduliwa na kuuliwa kwa Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya bado inatawaliwa na ukosefu wa amani na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyochochewa na uingiliaji wa nchi za kigeni.